KOCHA wa timu za soka za Taifa za wanawake, Bakari Shime amesema anaamini Twiga Stars itakwenda kutetea ubingwa wa mashindano ya Cosafa (Baraza la vyama vya soka Kusini mwa Afrika) yanayotarajiwa kuanza Agosti 31, Port Elizabeth, Afrika Kusini.
Akizungumza na gazeti hili jana, Shime alisema Twiga Stars ambao wamepangwa Kundi C na timu za Malawi, Botswana na Comoro watafanya vizuri kutokana na maandalizi aliyofanya.
“Tumefanya maandalizi mazuri na tutaanza kurusha karata ya kwanza kwa kucheza na Comoro Septemba 2 na nina imani tutatetea ubingwa maana sisi ndio mabingwa watetezi,” alisema Shime.
Alisema watahakikisha wanashinda michezo yote katika hatua ya makundi maana mshindi wa kwanza katika kila kundi ndio atafuzu nusu fainali na timu ya nne itakuwa mshindwa bora. Makundi yapo matatu. Baada ya mchezo dhidi ya Comoro, Twiga Stars itavaana na Botswana Septemba 5 na itamaliza hatua ya makundi Septemba 7 kwa kucheza na Malawi ambao walicheza nao fainali msimu uliopita.
Kundi A lina mwenyeji Afrika Kusini, Msumbiji, Angola na Mauritius na Kundi B lina timu za Lesotho, Zambia, eSwatini na Namibia.
Kwa mujibu wa ratiba, nusu fainali mshindi wa Kundi B atacheza na mshindi wa Kundi C na mshindi wa Kundi A atacheza na mshindwa bora na fainali itachezwa Septemba 11.
Tanzania hushiriki michuano hiyo kama mwalikwa na mara zote imekuwa ikifanya vizuri.