Shime Tanzania, Uganda bomba la mafuta liendelee

Kanisa Katoliki lapongeza ujenzi bomba la mafuta

SEPTEMBA 15,mwaka huu, Bunge la Umoja wa Ulaya lilipitisha azimio la kutaka kulazimisha Uganda, Tanzania na Kampuni ya mafuta ya Total Energies SE kuchelewesha utekelezaji Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) kwa madai kuwa unarudisha nyuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa nchi hizo.

Umoja huo umetoa wito kwa serikali za nchi hizi mbili kuanzisha hatua madhubuti kuhakikisha mamlaka, vyombo vya usalama na sera zinaheshimu na kuzingatia haki za binadamu.

Ni jambo la kufurahisha kwamba, serikali zote mbili; Uganda na Tanzania, zilibainisha msimamo wake wa kuendelea kutekeleza ujenzi wa bomba hilo.

Advertisement

Kauli zilizotolewa na viongozi wa Tanzania na Uganda kwa nyakati tofauti kwa kuweka bayana kwamba hakuna ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa na kuwa taratibu zote zinazohitajika zilifuatwa kabla ya mradi kuanza kutekelezwa, ni za faraja kubwa kila anayezitakia maendeleo nchi hizi.

Waziri wa Nishati nchini, January Makamba amethibitishia umma kwamba serikali imekuwa ikizingatia viwango vyote vya kimataifa katika utekelezaji wa mradi huo unaojengwa kutoka Hoima -Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.

Msimamo wa  Rais Yoweri Museveni wa Uganda, umezidi kukonga nyoyo kwa kutamka wazi kuwa dhamira ya kutekeleza mradi huo itaendelea kama ilivyopangwa kuhakikisha mafuta yanaanza kusafirishwa kama ilivyopangwa mwaka 2025.

Bila kujali kama EU imepitisha azimio hilo kupotoshwa au kwa sababu nyingine yoyote, Tanzania na Uganda  ziendelee kusimama kidete mradi uendelee kama ilivyokusudiwa.

Serikali zetu hizi mbili zisimamie msemo wa Kiswahili wa ‘kimfaacho mtu chake’ kutokana na ukweli kwamba mradi huu umeanzishwa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi wao na si wengine. Mradi unatoa fursa mbalimbali za kiuchumi na kibiashara katika hatua za awali ,  wakati wa ujenzi na wakati wa uendeshaji .

Katika hatua za awali, Watanzania wengi wamepata ajira sambamba na kampuni za kitanzania ambazo zimepata kazi  huku manufaa mengi na makubwa yakitarajiwa kupatikana kupitia mradi huu na kuchangia ukuaji wa uchumi.

Ni wazi kwamba, haiwezekani serikali zikaendesha mradi wa kuhujumu haki na maisha ya watu wake.  Ndiyo maana tunasema zina haki ya kutawala raslimali zake kwa kutekeleza mradi huu wa bomba la mafuta lenye urefu wa kilometa 1,443.

Lengo la mradi ni kuwezesha mafuta yatakayozalishwa Uganda kusambazwa katika soko la ndani na sehemu inayobaki kuuzwa nje kwenye soko la kimataifa kupitia bomba la mafuta; utekelezaji utakaoinua uchumi wa nchi hizi ambazo zote ni mwanachama wa Jumuiya ya  Afrika Mashariki.

Tunaungana na uamuzi wa Tanzania, Uganda kusimama kidete tukisimame kidete kwa kuhimiza utekelezaji wa mradi uendelee.

 

 

 

 

 

 

2 comments

Comments are closed.