Shinyanga kuwa kitovu cha umeme Kanda ya Ziwa

KISHAPU, Shinyanga: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko leo amezindua mradi mkubwa wa umeme jua utakaozalisha megawati 150 katika Kijiji cha Ngunga wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga ikiwa ni utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya kuibua, kuendeleza na kutekeleza vyanzo mbalimbali vya umeme ili kuondokana na utegemezi wa Maji na Gesi Asilia kuzalisha umeme.

Dk Biteko amesema mradi huo utaanza kuzalisha megawati 50 ifikapo mwezi Januari mwaka 2025 na hii ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuongeza vyanzo vya umeme kwani vilivyopo bado havitoshelezi mahitaji.

“Vyanzo vingine vya umeme tunavyoviendeleza ni pamoja na mradi wa Jotoardhi Songwe na Mbeya ambapo tarehe 1 Aprili mwaka huu uchorongaji unaanza katika eneo la Ngozi, mradi mwingine unaoenda kutekelezwa ni mradi wa megawati 100 wa upepo uliopo Makambako ambapo fidia imeanza kulipwa,” amesema Dk Biteko.

Ameeleza kuwa kutekelezwa kwa mradi huo mkoani Shinyanga, kunafanya Mkoa huo kuwa kitovu cha umeme katika Ukanda wa Ziwa kwani mpaka sasa kuna vituo vikubwa vitatu vya umeme ambavyo ni Ibadakuli, Bulyanhulu na Buzwagi ambavyo vinasambaza umeme kwenye mikoa mbalimbali nchini.

Habari Zifananazo

Back to top button