Shirika latoa msaada wa taulo kwa wanafunzi Kagera

KILA ikifika Mei 28 duniani kote huadhimishwa siku ya hedhi salama, ambapo kwa Mkoa wa Kagera, Shirika lisilo la kiserikali Agrithaman Foundation wameadhimisha siku hiyo kwa kuwapatia taulo za kike wanafunzi wa kidato cha tano wa shule ya wasichana Omumwani.
Mratibu wa shirika hilo anayeshughulikia maswala ya elimu ya lishe na hedhi salama, Mjumuzi Kibendera alisema hedhi salama inaendana na lishe bora, usafi wa mwili na mazingira rafiki kwa wanafunzi ili wajisikie salama.
Alisema shirika limeweza kutoa elimu ya hedhi salama pamoja na kuendelea kuandaa uchechemuzi wa kisera juu ya miundombinu safi ya kubadilishia taulo ,maji Safi na salama shuleni , pamoja na kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora.
Mwenyekiti wa wanafunzi anayeongoza klabu ya lishe bora katika shule ya Sekondari ya Omumwani , Farihia Hassan alisema kuwa shirika hilo limekuwa likitoa elimu juu ya kula vyakula bora, kuandaa mashamba darasa kupanda mbogamboga shuleni pamoja na elimu ya maswala ya Kidigitali juu ya kujua afua mbalimbali za lishe.
“Tunashukuru kupata taulo za kike mara nyingi pia tunatumia vitambaa vya kufua tunaendelea kuwaomba wadau waendelee kujitoa na kutusaidia taulo za kike , Agrithaman wanatupatia Elimu ya lishe kwa vitendo tunalima mbogamboga tunatumia pia na walimu wetu ,tunafundishwa usafi hivyo tunajisikia fahari sana kuwa wadau wa Agrithaman ambao kiukweli wanatulea sawasawa “alisema Hassan.
Mwalimu wa shule hiyo, Leonia Sevrine alisema wanafunzi wengi wanakabiriwa na changamoto ya kukosa baadhi ya vipindi kutokana na kuumwa tumbo ,ambapo shule hiyo imekuwa ikishughulikia changamoto za wanafunzi ambao wanapata tatizo la kuumwa tumbo.
Kwa mjibu wa tafiti zilizofanywa na Shirika la aSNV Netherlands Development pamoja na Tanzania Water and Sanitation Network (TAWASANET) katika halmashauri 16 nchini Tanzania mwaka 2015 inaonyesha kuwa asilimia 48 ya wanafunzi ukosa baadhi ya vipindi vyao kila mwezi kutokana na kuwa katika mzunguko wa Hedhi Hali ambayo uadhiri uwezo wao wa kufikiri kwa ufasaha.