‘Shirikianeni na serikali vita dawa za kulevya’
Dodoma: WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewatakwa viongozi wa dini kushirikiana na serikali katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Majaliwa ameyasema hayo leo Septemba 28, 2023 akihutubia Baraza la Maulidi Kitaifa katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Amesema viongozi wa dini wana nafasi kubwa ya kuelimisha jamii, kukemea vitendo viovu na kuhimiza ushirikiano na kujali ustawi wa jamii.
“Nawapongeza kwa kazi kubwa mnayofanya, mnashirikiana na serikali kila mnapohitajika kwa kutoa hamasa kwa waumini na Watanzania, serikaili imekuwa ikishirikiana na viongozi wa dini katika kampeni mbalimbali ambazo zimeleta matokeo mazuri,” amesema Majaliwa na kuongeza:
“Kutokana na ukweli huo naomba niwasihi sana endeleeni kushirikiana na serikali katika masuala muhimu kwa mustakabali wa nchi yetu, sambamba na kuendelea kutoa mafundisho ya kiroho, shirikianeni na serikali kusisitiza masuala ya kimkakati kama mapambano dhidi ya dawa za kulevya,” amesema.
Amesema, biashara ya dawa za kulevya na matumzi ya dawa hizo haramu imekuwa kubwa duniani na Tanzania imepitiwa na wimbi hilo.
“Dawa za kulevya siku za nyuma ilizoeleka maeneo ya mjini lakini sasa hata vijijini tatizo linaenda, vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa wameathirika zaidi, hata baadhi ya watoto wetu wapo kwenye hatari kubwa kutumbukia katika wimbi hili kutokana na ushawishi rika, na kutojua madhara,” amesema.
Pia amesema dawa za kulevya zina athari kiuchumi, kiafya na kijamii.
Afya ya akili:
Amesema matumizi ya dawa za kulevya yana athiri uwezo wa kufikiri kwa mtumiaji na husababisha tatizo la afya ya akili.
“Niwasihi sana viongozi wangu, kama ambavyo tumeshirikiana katika mambo mbali mbali tushirikiane katika mapambano ya dawa za kulevya…
“Tuondokane na tatizo hili kwa kuwa kauli yenu inakubalika na waumini na Watanzania wote, mmekua mkijenga utii wa sheria bila shuruti, ” amesisitiza Majaliwa.