SHIRIKISHO la Umoja wa Machinga Tanzania (SHIUMA) limetangaza kumvua madaraka naibu katibu mkuu wake, Joseph Mwanakijiji na kumzuia kufanya shughuli zozote zinazohusiana na taasisi hiyo mahali popote nchini.
Tangazo la kumng’oa katika nafasi hiyo limetolewa leo na uongozi wa shirikisho hilo ambao umekuja mjini Iringa kushughulikia na kumaliza changamoto za uongozi wa machinga wa mjini Iringa na kiini cha migomo na maandamano ambayo wamekuwa wakiyafanya mara kwa mara.
Akitangaza uamuzi huo leo, Katibu wa SHIUMA Taifa, Venatus Magayane alisema; “Kamati Kuu ya SHIUMA iliyokutana hivi karibuni imejiridhisha pasipo shaka kwamba Joseph Mwanakijiji amakosa sifa za kuendelea kuwa Naibu Katibu Mkuu wa SHIUMA kwasababu ya mienendo yake.”
Alisema akiwa Naibu Katibu Mkuu ameshindwa kuinadi SHIUMA na Katiba yake kwa machinga wa Iringa pamoja na kwamba kwa kupitia shirikisho hilo amekwenda mikoa mbalimbali nchini kulitangaza shirikisho hilo.
Baada ya kufuatilia migogoro na vurugu za mara kwa mara zilizokuwa zikifanywa na machinga wa Iringa alisema wamebaini kiongozi huyo alikuwa sehemu yake kinyume na katiba ya SHIUMA.
Awali Mwenyekiti wa SHIUMA, Matondo Masanja aliutangaza uongozi wa muda wa SHIUMA Iringa Mjini akisema utakuwa na wajibu wa kuwaunganisha na kuwasajili machinga katika shirikisho hilo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa viongozi wake.
Aliwataja viongozi hao kuwa ni pamoja na Kessy Dandu anayekuwa Mwenyekiti, Frank Mwambepali Makamu Mwenyekiti, Katibu Abubakar Sadick, Naibu Katibu Falahani Ismail, Mweka Hazina Ibrahim Bakari na Maneno Nyambuya Afisa Habari.
Aliwataja watakaokuwa wajumbe wa uongozi huo kuwa ni Aloyce Adeltus, Anna Sanga, Zakaria Amani, Esau Sanga, Abuja Peter, Ashura Ramadhani, Khalifa Abdalla na Allen Kilewela.
Masanja alitoa onyo kwa uongozi huo akisema atakayebainika kuhamasisha vurugu,maandamano na migomo inayohatarisha amani na usalama wa mali na raia wengine atachukuliwa hatua za kisheria.
“SHIUMA ni chombo kinachofanya kazi na serikali katika kuwaendeleza machinga na biashara zao. Jambo lolote linaloleta tofauti baina ya pande hizo mbili litamalizwa kupitia meza ya majadiliano na sio kwa kuhamasisha vurugu au maandamano,” alisema.
Akifungua mkutano huo, Katibu Tawala wa Wilaya ya Iringa, Michael Semindu alisema serikali itafanya kazi bega na viongozi hao wa muda mpaka watakapopatikana viongozi wa kudumu.
“Tulikwishaanza kuzishughulikia changamoto mbalimbali za Machinga hususani wa soko la Mlandege, niahidi zilizobaki tutazimaliza tukiwa na uongozi huu mpya wa machinga,” alisema.
Alizungumzia pia ujenzi wa ofisi ya machinga akisema itakayojengwa Iringa itakuwa ya mfano kwani itakuwa na ukumbi wa mikutano pamoja na ofisi zingine za makundi ya bajaji, daladala na afisa mmoja wa serikali anayeshughulikia biashara.
Comments are closed.