KATAVI: Wavuvi wilayani Tanganyika Mkoa wa Katavi wamekubali mpango wa serikali wa kuhuisha uvuvi ndani ya miezi mitatu katika Ziwa Tanganyika ili kupisha samaki kuzaliana katika ziwa hilo.
Wakizungumza mbele ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti katika mkutano wa hadhara na wadau wa sekta ya uvuvi Kata ya Ikola, wamekiri kuwa samaki kwa sasa wameadimika hivyo kama mpango huo utaongeza mazao ya samaki ziwani wako tayari kupisha mpango huo.
“Na umri wangu nilionao mimi, ninaamini sasa hivi kwamba mazao ziwani yametoweka,sijui ni ongezeko la watu, sijui ni uvuvi ambao tunaufanya ambao ni nje na utaratibu lakini wataalamu wamekwisha tazama na wameona wametuletea utaratibu wa sisi tujaribu kufunga ziwa ili tuone mafanikio ya baadae” -Amesema mmoja wa wavuvi.
Awali, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Alexander Mnyeti akiwasilisha mpango huo wa kulifunga ziwa Tanganyika kwa wadau wa uvuvi amesema hayo ni makubaliano ya mkataba baina ya nchi nne ambazo zinalizunguka Ziwa Tanganyika uliosainiwa mwaka jana lengo likiwa ni kunusuru upotevu wa mazao yanayopatikana katika ziwa hilo hususani samaki.
Mnyeti amesema, usitishwaji wa shughuli za uvuvi Ziwa Tanganyika utakuwa wa miezi mitatu kuanzia Mei 15 hadi Agosti 15 mwaka huu na kuongeza kuwa sababu za kusitisha uvuvi ndani ya miezi hiyo ni kutokana na utafiti uliofanywa na wataalamu na kugundua kuwa hiyo ni miezi ambayo samaki huzaliana na vifaranga kukomaa.
Serikali imetenga zaidi ya Shilingi bilioni 20 ambazo zimetengwa kwa ajili ya kununua vizimba takribani 800 kwa ajili ya wavuvi wa Ziwa Tanganyika na Ziwa Victoria ambavyo vitakabidhiwa kwa wavuvi ambao watakuwa katika vikundi ili viwe mbadala wakati shughuli za uvuvi zitakapositishwa kwa muda katika maziwa hayo.
Hata hivyo, shughuli za uvuvi zitaendelea katika mabwawa na mito.