TEA kuboresha miundombinu shule 26 mitaala mipya

MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA), imejipanga kutoa vifaa na kuboresha miundombinu kupitia mfuko wa elimu kwa shule 26 zitakazofanyiwa majaribio ya mtaala mpya mwakani.

Kaimu Mkurugenzi wa Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Masozi Nyirenda amesema hayo alipozungumza na HabariLeo mkoani Dar es Salaam.

“Katika shule karibu 26 za awali zitakazofanyiwa majaribio ya mtaala mpya kuanzia Januari, uhitaji mkubwa umejikita katika masuala ya uboreshaji wa miundombinu na vifaa vya kujifunza na kufundishia ambapo ndio eneo letu.

“Tunajipanga kuwekeza zaidi kuhakikisha kuwa shule zote zitakazoanza watapata vifaa lakini pia kuboreshewa miundombinu kupitia mfuko wa elimu lakini pia tutahamasisha wadau wengine kuweza kufadhili miradi kama hiyo,” amesema.

Amesema Mfuko wa elimu ulianzishwa kwa sheria na 8 ya mwaka 2001 na sheria ya bunge katika sheria hiyo hiyo ilianzisha Mamlaka ambayo inasimamia mfuko huo.

Amesema TEA imekuwa ikisimamia mfuko wa elimu ambao una majukumu makubwa mawili ambayo ni kutafuta rasilimali kutoka vyanzo mbalimbali kutoka kwa wadau mbalimbali,

Pamoja na kupanga na kutoa rasilimali hizo kuelekea katika sekta ya elimu katika miradi mbalimbali ya elimu katika kuboresha usawa lakini pia kuweka ubora wa elimu nchini.

Amesema wamekuwa wakifadhili miradi mbalimbali kuanzia ngazi ya elimu ya awali mpaka vyuo vikuu kwa Tanzania Bara, kwa Zanzibar wanafadhili miradi ya elimu ya juu pekee kulingana na sheria ya Muungano.

Katika hatua nyingine amesema wamepokea maoni mbalimbali kutoka kwa wanafunzi, walimu, wadau wa vyuo vya elimu ya juu na wananchi kuhusu namna ya kuboresha huduma za mfuko huo.

Amesema maoni wameyapokea katika maadhimisho ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), ambayo walishiriki kwa kuwa ni wadau wa elimu.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za mamlaka TEA, Mwanahamisi Chambega amesema wanahamasisha wananchi mmoja mmoja na wadau wa elimu kuchangia mfuko wa elimu kupitia mamlaka hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button