SERIKALI imepongeza shule binafsi ambazo hazina kawaida ya kuchuja wanafunzi unapofikia muda wa mitihani ya kitaifa ikiwemo St Anne Marie Academy.
Pongezi hizo zilitolewa mwishoni mwa wiki na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa ambaye alimwakilisha Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kwenye mahafali ya 18 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari St Anne Marie Academy ya Mbezi kwa Msuguri.
Alikemea tabia ya ubaguzi unaofanywa na baadhi ya shule kwa lengo la kuongeza ufaulu kwenye mitihani ya kitaifa jambo ambalo alisema ni ubaguzi mkubwa.
Aidha, alisema hatua ya kubagua wanafunzi wakati wa mitihani ya kitaifa ni ukatili mkubwa na fedheha kwa wazazi ambao wamejinyima na kutumia fedha nyingi kuhakikisha mtoto wao anapata elimu.
Aliwapongeza walimu wa shule hiyo kwa ubunifu mkubwa walioonesha wa kutengeneza bidhaa mbalimbali kama sabuni hali ambayo itawawezesha kuwa wajasiriamali baada ya masomo yao.
Aliwataka wazazi wawafundishe watoto wao ujasiriamali kama njia ya kujitafutia kipato siku zijazo huku akiwataka wenye shule kufundisha lugha mbalimbali ikiwemo Kichina, Kiarabu na Kifaransa kwani yana soko kubwa.