SHULE mbili za msingi Reginald Mengi na Ubungo NHC, zimependekezwa kuwa za mchepuo wa kiingereza na Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam.
Halmashauri hiyo mpaka sasa imekuwa haina shule za mchepuo huo, tofauti na halmashauri nyingine mkoani Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa amesema hayo leo katika Kikao cha Kuwasilisha Rasimu za Mpango na Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 na mpango wa muda wa kati 2024/25 -2026/2027.
Ntiruhungwa amesema katika ulimwengu wa sasa, Manispaa kukosa shule ya mchepuo wa kiingereza sio sawa ndio maana imejipanga kuwa nayo.
Amesema tayari ameshaandika barua Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ( Tamisemi), kuhusuana na jambo hilo.
“Ninaimani barua ikijibiwa itakuwa imeridhia,” amesema.
Ameleza tayari kuna fedha wametenga kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo mbili, zikishaidhinishwa na tamisemi, watazitumia.
Amesema katika eneo la shule ya Ubungo NHC, watajenga vyumba vinne kwa ajili ya kufundishia.
Awali Mkuu wa Wilaya hiyo. Hashim Komba amesema ifike mahali wasaidie wana Ubungo ambao wanataka kusomesha watoto wao kwenye mchepuo wa kiingereza.
“Ndoto hii itimie isiwe maneno. Hii ndiyo alama tunayoweza kuacha,” amesema.