SERIKALI imetoa Sh milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Msingi Kawambwe iliyopo Halmashauri ya Tanganyika mkoani Katavi yenye wanafunzi 160, ambao wanalazimika kusomea chini ya kibanda cha nyasi.
Shule hiyo ilianzishwa kutokana na wanafunzi wa eneo hilo kushindwa kuhimili kutembea umbali mrefu kufuata masomo.
Hali hiyo iliwafanya wakazi wa kitongoji cha Inyagantambo, Kijiji cha Majalila Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, kuanzisha ujenzi wa shule ya Msingi Kawambwe kunusuru watoto wanaotembea umbali mrefu kufuata masomo katika Kijiji cha Majalila na Vikonge, huku serikali ikiwaunga mkono jitihada zao.
Wazazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika wameamua kuanza kuchimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, huku serikali ikiahidi kukamisha madarasa hayo haraka, ili kutatua changamoto iliyopo.
“Tulikubaliana kwenye kikao kujenga shule hapa karibu kwa kuwa watoto wetu waliteseka sana kufuata masomo mbali na kijiji chetu,” amesema Zuwena Said mwananchi wa Kitongoji cha Inyagantambo.
Nao walimu pamoja na wanafunzi wamewashukuru wazazi pamoja na serikali kwa kusikia kilio chao, huku wakiamini kukamilika kwa ujenzi huo wanafunzi watasomea sehemu nzuri na uelewa utaongezeka.
“Mvua ilipokuwa ikinyesha tunapata changamoto sana, huwezi ukafundisha lazima utafute namna ya kuwakinga watoto mpaka mvua itakapokata,” amesema mwalimu Erick Ruben.
“Mvua ikinyesha tunalowana na madaftari yanalowana na hata msimu wa jua pia linatupiga, ila tunashukuru ujenzi huu ukikamilika tutasoma vizuri,” amesema Zainab Ramadhan ambaye ni mwanafunzi wa shule hiyo.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Inyagantambo, Peter Christopher amesema serikali imewaunga mkono baada ya wao kuona watoto wanateseka, huku Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu akisema ushirikiano wa wananchi hao umesaidia kuokoa gharama za uchimbaji wa msingi.
“Kilio chao kikamfikia Rais Dk Samia Suluhu Hassan, amewaletea Sh milioni 200 ambazo zitajenga madarasa sita pamoja na nyumba ya mwalimu yenye thamani ya Sh milioni 28, vyoo matundu 10 yenye thamani ya Sh milioni 22,” amesema Mkuu huyo wa Wilaya.
Aidha Buswelu amesema katika Wilaya ya Tanganyika wanatarajia kujenga shule mpya sita kwa fedha zilizotolewa na serikali kuu na fedha za mradi wa BOOST.