Shule yaomba kujengewa madarasa, vyoo

UONGOZI wa shule ya Sekondari ya Igogwe iliyopo kata ya Bugogwa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza umeuomba Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) na wadau maendeleo ya jamii kuwasaidia katika ujenzi wa madarasa nane pamoja na matundu ya vyoo sita.

Ombi hili limetolewa leo na makamu mkuu wa shule ya Sekondari Igogwe, Innocent Mashauri wakati wa kutembelea miradi mbalimbali ya TASAF Wilaya ya Ilemela.

Amesema mwaka 2024 wanatarajia kupokea wanafunzi 300 watakaojiunga na kidato cha kwanza. Mashauri amesema shule yao kwa sasa ina wanafunzi 334 kwa kidato cha kwanza na cha pili.

“Naishukuru sana TASAF kwa kuweza kutujengea vyumba vya madarasa manne na matundu ya vyoo. Nawashukuru pia TASAF wameweza kutujenga jengo la utawala katika shule yetu” amesema.

Ameuomba mfuko huo na wadau wengine wa maendeleo kuwasaidie katika ujenzi wa bwalo kwajili ya chakula pamoja na ujenzi wa nyumba 11 za walimu. Amesema ujenzi wa bweni katika shule ya utasaidia sana kuongeza ufaulu katika shule yao na kuondoa changamoto ya mimba.

Naye mratibu wa TASAF, Leonard Robert amesema katika mwaka wa fedha 2021/2022 walipokea Sh milioni 500 kutoka TASAF kwajili ya utekelezaji wa miradi nane.

Amesema kupitia pesa za miradi ya Tasaf wamefanikiwa kujenga jengo la utawala moja, maabara za sayansi na bweni moja la wasichana katika shule ya sekondari Bugogwa.

Amesema miradi ya Tasaf inafaida sana kwakuwa awali shule ya Igogwe ilikuwa na madarasa matano tu lakini sasa Tasaf imejenga madarasa manne.

Naye mkuu wa kitengo cha Habari na Mawasiliano kutoka TASAF makao makuu Zuhura Mdungi amesema TASAF itaendelea kusistiza ushiriki wa jamii katika kuleta maendeleo. Mdungi amewapongeza wakazi wa kata ya Bugogwa katika ushiriki wao wa ujenzi wa miundo mbinu mbalimbali katika shule ya sekondari ya Igogwe.

Habari Zifananazo

Back to top button