Shule yapewa kompyuta Iringa

SHULE ya Sekondari Mtwivila ya mjini Iringa imenufaika na msaada wa vifaa vya TEHAMA vyenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 89 vilivyotolewa na taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation kwa kushirikiana na African Child Projects (ACP) kwa kupitia mradi wa uunganishwaji wa shule kidigitali.

Mradi huo wanaoutekeleza kwa kushirikiana pia na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) unalenga kuziunganisha shule 300 nchini kote.

Akipokea na kuzindua vifaa hivyo Mkuu Wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amezishukru taasisi hizo kwa kuwezesha mradi huo ambao mpaka sasa umezinufaisha shule 14 mkoani mwake.

Katika kuunga mkono maendeleo hayo, Dendego ameziagiza halmashauri zote za  mkoa huo kuanza kutenga bajeti maalum kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya Tehama ili kuwawezesha wanafunzi katika shule zote kusoma pia kwa kutumia kompyuta.

Aidha Dendego amewataka wanafunzi wanaonufaika na vifaa hivyo vya kidigitali kuvitumia kwa malengo na manufaa yaliyokusudiwa badala ya matumizi ya mtandao yasiyofaa.

Akikabidhi vifaa hivyo Meneja wa Vodacom Nyanda za Juu Kusini Happiness Shuma alisema msaada huo utaiwezesha shule hiyo kuwa na kituo cha kompyuta na kutoa mafunzo kwa wanafunzi wa shule hiyo ili wapate ujuzi wa teknolojia ya habari na mawasiliano.

Alisema lengo la Vodacom ni kuhakikisha wanafunzi katika shule za mkoa wa Iringa pia wananufaika na mradi huo unaotekelezwa kwa awamu katika maeneo mbalimbali nchini ili wapate ujuzi wa kutumia Tehama.

Alisema Vodacom Tanzania Foundation ina historia ya kuwa na miradi ya elimu nchini Tanzania kwa miaka kadhaa sasa na imekuwa ikijitahidi kuleta mawazo bunifu kwenye suala zima la kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watoto na vijana katika jamii zenye uhitaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Shule ya Sekondari Mtwivila, Dainess Myala alishukuru kwa msaada huo akisema utasaidia kuwaondoa wanafunzi wake katika giza la matumizi ya TEHAMA.

“Tutahakikisha vifaa hivi vinawanufaisha wanafunzi wengi ili kutimiza lengo namba tisa la malengo ya maendeleo endelevu (SDG’s) linalolenga kuongeza kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa huduma za TEHAMA pamoja na lengo namba nne linalolenga kunakuwepo usawa katika ubora na upatikanaji wa elimu ili kujenga mazingira endelevu ya kujifunza kwa wote,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button