”Si mwanaume kamili”

Imani potofu yatajwa kama kisababishi kikuu

TAKWIMU za umoja wa mataifa za mwaka 2022 ya Matarajio ya Idadi ya Watu Duniani imetaja, Afrika ya Mashariki  kuwa  eneo linaloongoza katika  ukuaji wa  idadi ya watu  barani Afrika ikiwa na watu zaidi ya milioni 457.

Kukabiliana na hali hiyo, Shirika la Afya Duniani, (WHO), pamoja na jamii ya umoja wa mataifa bado zimeendelea kusisitiza umuhimu wa  uzazi wa mpango, kwa kushauri wanaume kujiunga kwa kampeni hiyo  kwa kutumia mpira au kukata mshipa wa uzazi maarufu vasectomy

Kutokana na hali hiyo, HabariLeo imefanya mahojiano na wataalamu wa afya ya uzazi ambao wanasema mwitikio mzuri wa uzazi wa mpango upo kwa wanawake kuliko wanaume na hiyo inatokana na imani potofu ambayo imejengwa ndani ya jamii.

Daktari kutoka Maria Stopes Ritha Chuwa anasema baadhi ya watu wanafikiri kuwa hautakuwa mwanaume kamili baada ya kufanyiwa upasuaji.

Dk Ritha anasema asilimia ndogo sana ya wanaume wa kiafrika wamefunga uzazi, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa mataifa ya mwaka 2013

Nchini Afrika Kusini na Namibia idadi ni kubwa kwa asilimia 0.7  na asilimia  0.4,  Duniani kote  ni asilimia 2.2  ya wanaume wamefunga uzazi ukilinganisha na asilimia 18.9 ya wanawake waliofunga uzazi.

Anasema, njia kubwa ya uzazi wa mpango inayotumiwa na wanaume ni Condom na wachache ndio ufanya vasectomy.

“Tunatumaini tukimprove katika suala la uzazi wa mpango, nchi itaendelea, kipato cha mtu mmoja mmoja kitaimarika, tatizo vijana ambao wapo kula tu bila kufanya kazi litapungua.

“Ukitumia njia ya uzazi wa mpango, kama ulikuwa ‘active’ utakuwa ‘active’ awe ni mwanamke au mwanaume haidhuru utafanya tendo la ndoa kama kawaida.”Anasema Dk Ritha

Anasema mwitikio wa wanaume upo chini ya asilimia 3, kutokana na uoga, katika utamaduni wa kiafrika wanadhani kukatawa uume ni kupoteza uanaume wako, lakini ni kuzuia mbegu zisipitwe.

“Waafrika wengi wakiwemo Watanzania wana ile imani ya kuwa na watoto wengi ni kama baraka, wao wanakuwa ‘proud’ ndio inachangia watu kutokubali hiyo njia.

Hata hivyo, anasema wanaume kutumia njia ya uzazi wa mpango sio kupoteza uume wao kwani haitumii kemikali ni upasuaji mshipa unafungwa ‘procedure’ ambayo  haichukui muda mrefu

Upasuaji wowote unaofanyika kwenye mwili wa binadamu ni kama yupo safari, mtu anapokuwa safari gari muda wowote inaweza kupata pancha, sio asilimia kubwa. Chakuzingatia ni  kupata ushauri wa mtaalum kabla maji kuyavulia nguo,

Nae, Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Dk Beatus Nyamuhiba kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Amana jijini Dar es Salaam anasema, wanaume wengi hawana ufahamu kuhusu uzazi wa mpango na hasa ‘vasectomy’

”Watu wengine wanafananisha na kuhasiwa, kwa kuwa wanafikiri viungo vyote vinakatwa na kubaki kama mwanamke,” anaeleza Dk Beatus mtaalamu wa masuala ya ufungaji uzazi kwa njia ya upasuaji.

Hii ni tofauti na mataifa tajiri kama Canada, ambapo mwaka 2013 Umoja wa mataifa ulibaini kuwa asilimia 22 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa ambao wameolewa wako na wanaume waliofunga uzazi kama njia ya uzazi wa mpango. Nchini Uingereza ni asilimia 21, New Zealand ilikuwa asilimia 19.5 na Marekani ilikuwa asilimia 11.

Amesema, kwa Tanzania muitikio mkubwa wa wanaume kufanya ‘vasectomy’ upo katika Mikoa ya Kigoma na Mwanza huku Dar es Salaam hali ikiwa mbaya.

“Elimu zaidi iendelee kutolewa hususani kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambayo hali ni mbaya, wanaume wengi hawapo tayari kufunga na wengine ni kwa sababu na imani potofu ambazo wameaminishwa mtaani.”Anasema na kuongeza

“Shida kubwa iliyopo wanaume wengi wanadhani ukishafanya vasectomy ngoma haisimami tena, watu wanaelewana wenyewe kwa wenyewe mtaani, hukija mtoa huduma ukawaelewesha kitaalamu hawakuelewi.”Amesema

Anasema njia ya kufunga uzazi kwa wanaume ni njia ya uzazi wa mpango ambayo hufanywa kwa njia ya upasuaji kukata au kufunga mirija inayosafirisha mbegu za uzazi za mwanaume, ili kuzuia mwanamke asipate mimba.

“Upasuaji mara nyingi hufanywa kwa muda wa dakika takriban 15, mgonjwa huwa macho lakini hapati maumivu yeyote. Njia hii inafanya kazi ya kuzuia mimba kwa silimia 95.” Anasema

Anasema njia ya kufunga uzazi kwa wanaume haiathiri nguvu za kiume au uwezo katika tendo au kulifurahia tendo.

“Mwanaume ataweza hayo yote,isipokuwa hataweza kumpa mwanamke ujauzito,”anasema.

Njia hii haizuii wala kukinga  mwanaume dhidi ya maradhi ya zinaa, kuna mipira ya kiume ambayo inaelezwa kuwa njia ya kuaminika kwa asilimia 98 ikiwa itatumika vyema.

RIPOTI YA WHO YA MWAKA 2019

Ripoti  ya Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema njia za uzazi wa mpango ni muhimu katika kuzuia mimba zisizopangwa na tafiti zinaoyesha kuwa, asilimia 85 ya wanawake walioacha kutumia njia hizo wamepata ujauzito katika miaka ya mwanzo.

Miongoni mwao waliokumbwa na mimba zisizotarajiwa na kuamua kuzitoa, waliacha kutumia njia za uzazi wa mpango kwa hofu ya afya zao, madhara ya njia hizo na changamoto za matumizi.

Takwimu zinaonesha kuwa duniani kote wanawake milioni 74 wanaoishi kwenye nchi za kipato cha kati na chini kila mwaka hupata mimba zisizotarajiwa.

WHO inasema hali hiyo inasababisha milioni 25 kutoa ujauzito kwa njia zisizo salama hali inayosababisha vifo 47,000 kila mwaka.

MWANAUME SHUJAA

Julias Jackson anajishughulisha na kilimo cha mpunga, viazi na mahindi, yupo Sengerema mkoani Mwanza.

Julius ana mke na Watoto watano, ni mwanaume shujaa ambaye HabariLeo ilikumkuta akipata elimu ya afya ya uzazi katika kituo cha Katunguru wilayani Sengerema

Akizungumza anasema “Mimi na mke wangu kabla hatukuwa tunatumia njia ya uzazi wa mpango baada ya kusikia mafunzo tukaamua kutumia njia ya uzazi wa mpango.

‘Natumia condom ambayo ni salama zaidi na rahisi kuipata, tunatumia kondomu mimi na mama hakuna shida wala hakuna aibu.

FAIDA YA NJIA YA UZAZI WA MPANGO:

Julius anasema,  faida  kubwa  aliyoipata baada ya  kutumia njia ya uzazi wa mpango ni mama kupumzika kupata mimba za mara kwa mara, yupo huru sio kila mwaka kuzaa, mtoto anakuwa na afya njema na imemsaidia kuwa na nafasi ya kufanya kazi, mke wake  anakuwa na afya njema na wanazalisha kwa wingi vyakula

DHANA POTOFU:

“Nilikuwa natishwa condom zina vimelea mama anaweza kupata saratani ya kizazi, baada ya kupata elimu tukaona yote hayo ni uongo ni kudumaza akili;….. “Mimi kama mwanaume niliamua kutumia condom kwa vile ni njia rahisi, madukani zinapatika hata kwa sh 200 au 300 na nilianza kutumia uzazi wa mpango tangu  mwaka 2000.” Anasema

 TAKWIMU ZA UZAZI WA MPANGO TANZANIA

Kwa mujibu wa takwimu za Tanzania zilizowasilisha kwenye bunge la bajeti la mwaka wa fedha 2023/2024 zinasema katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 Serikali ilinunua na kusambaza vidonge vya uzazi wa mpango 2,538,247 sawa na asilimia 89 ya lengo. Sindano za uzazi wa mpango aina ya Depo-provera dozi 2,564,691 sawa na asilimia 94 ya lengo na vipandikizi 552,494 sawa na asilimia 81 ya lengo.

Aidha, katika kipindi cha taarifa hiyo jumla ya wateja 4,509,605 walitumia njia mbalimbali za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganishwa na wateja 4,905,854 kipindi kama hicho mwaka 2021/2022.

Taarifa za Uendeshaji wa Huduma za Afya (MTUHA) zinaonyesha kuwa njia za uzazi wa mpango ambazo zilitumika katika kipindi cha Julai 2022 hadi Machi 2023 ni pamoja na vipandikizi (asilimia 45.7); Sindano (asilimia 22.8); vidonge (asilimia 12.6); kondomu (asilimia 11.6), vitanzi (asilimia 5.9); kufunga kizazi (asilimia 0.6); na njia nyingine (asilimia 0.9).

Aidha, katika kipindi hicho, jumla ya wateja wapya 3,491,989 sawa na asilimia 60.7 ya wanawake walio wa umri wa kupata ujauzito waliotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango ikilinganishwa na wateja 3,049,011 sawa na asilimia 62.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2021/22.

 

Habari Zifananazo

Back to top button