Siasa, soka inavyounganisha jamii

MBUNGE wa Jimbo la Kalenga Jackson Kiswaga ametumia uhusiano kati ya mpira wa miguu na siasa kuwafikia wapiga kura wake zaidi ya 100,000 katika kipindi cha siku 60 tu.

Kwa kupitia mashindano ya Kombe la Kiswaga (Kiswaga Cup) yaliyoshirikisha timu 30 kutoka kata 15 za jimbo hilo, mbunge huyo amedhihirisha jinsi matukio ya michezo yanavyoakisi masuala ya kisiasa na kijamii katika eneo husika.

Timu ya Chamgogo FC imeibuka mshindi wa ligi hiyo iliyofanyika kwa mtoano baada ya kuibwaga Kidamali FC kwa magoli 2-1 katika fainali iliyopigwa ndani ya dimba la Kalenga jimboni humo.

Nafasi ya tatu ya michuano hiyo inayozidi kujizolea umaarufu kwa wananchi wa jimbo hilo na vitongoji vyake ilikwenda kwa Ugwachanywa FC baada ya kuitwanga bila huruma timu ya Muwimbi Fc kwa mabao 4-0.

Wakati mshindi wa kwanza wa ligi hiyo iliyodhaminiwa na mbunge huyo kwa zaidi ya Sh milioni 28 alijipatia fedha taslimu Sh Milioni moja pamoja na kikombe, mshindi wa pili aliondoka na Sh 800,000 huku wa tatu akikomba Sh 600,000.

Pamoja na zawadi hizo, mshindi wa kwanza atafanya ziara ya siku tatu katika visiwa vya Zanzibar kupitia mwaliko uliotolewa na Katibu wa NEC Oganaizesheni, Issa Haji Gavu kama zawadi yake kwa mshindi huyo huku Kiswaga mwenyewe akiahidi kuwapeleka bungeni miamba hao wakombe hilo.

Akiwakabidhi zawadi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Verronica Kessy alisema; “Ili kuelewa uhusiano kati ya michezo na siasa, mtu lazima kwanza aelewe uhusiano kati ya michezo na jamii.”

Kessy alisema michezo ni kama taasisi ambayo mwelekeo wake ni kuibua hali ya kijamii iliyopo na inaweza kufanya kazi kwa niaba ya wanasiasa au vyama vya siasa.

Alisema viongozi, watawala, na watu wenye mamlaka mara nyingi wametumia michezo kusisitiza utawala wao wa kisiasa.

Kiswaga mwenyewe alisema wanasiasa wanaweza kuandaa matukio ya michezo kama vile mashindano ya mpira wa miguu kwa lengo la kuwavutia wapiga kura kushiriki au kuhudhuria matukio hayo.

Alisema matukio kama haya yanaweza kutumiwa kama fursa ya kujadili sera za kisiasa na kushirikisha wapiga kura.

Kiswaga mwenyewe aliahidi kuendelea kudhamini ligi hiyo huku akisema atahakikisha anaiboresha kila mwaka ili hadhi yake iwe ya kitaifa.

Alisema kwa kupitia michezo wanasiasa na serikali yenyewe wanaweza kutoa ahadi ya kujenga miradi mbalimbali ya kijamii, kuibua na kuendeleza vipaji, kujenga afya na kuwaunganisha vijana kupitia mazoezi.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x