SHIRIKA la Kuendeleza Viwanda Vidogo (SIDO) kwa kushirikiana na Mgodi wa Bucreef imekuja na mradi wa kuwezesha wajasiliamali Halmashauri ya Wilaya ya Geita kupiga hatua kupitia kilimo biashara.
Akizungumuzia katika semina ya mradi huo iliyofanyika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Katoro, Meneja wa SIDO mkoa wa Geita, Nina Nchimbi ameeleza wameanza na wajasiliamali wanaopakana na mgodi.
Amesema wameanza na kina mama wakazi wa kijiji cha Mnekezi, na baadaye watapambana kuwafikia wajasiliamali wote kata ya Kaseme na halmashauri ya mji wa Geita ili waweze kufanya biashar na mgodi.
“Tunataka kuona ni namna gani tunapeleka taarifa hizi sahihi jamii iweze kuelewa na kujua ndani ya migodi inayotuzunguka kuna fursa gani, na pia ndani ya migodi inayotuzunguka wanatuachia nini.
“Pia hapa kuweza kuona jamii yetu inapata elimu ya kutambua fursa zilizopo ndani ya mkoa wetu, na sisi tunajitoa zaidi kuweza kuona jamii yetu inatambua vizuri na kuelewa na kutumia fursa tulizonazo.
“Vikundi ambayo tumekutana nao sasa hivi vitajikita zaidi kwenye ufugaji wa kuku, ufugaji wa mbuzi pamoja na unenepeshaji lakini vilevile kilimo cha mbogamboga na matunda.”
Amesema kupitia mgodi wa Bucreef wanatarajia kuhakikisha wajasiliamali wadogo hasa kina mama wananufaika moja kwa moja na elimu ya ujasiliamali, kupatiwa masoko na mikopo kutoka SIDO .
Ofisa Raslimali Watu Mgodi wa Bucreef, Domitira Damas amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uwezo wajasiliamali kuzalisha bidhaa zenye kiwango na misingi bora ya kufanya biashara na mgodi.
“Mafunzo haya yatawapa uelewa zaidi kwa sababu watu wamezoea kufanya kilimo ambacho siyo cha biashara kwa hiyo kupitia mafunzo haya wataelewa tofauti ya kilimo cha nyumbani na kilimo biashara.”
Mjasiliamali, Regina Matonange amesema mradi huo utawasaidia kuongeza thamani ya bidhaa zao na kuziuza Bucreef kwani awali waliona kufanya biashara na mgodi huo ni ndoto isiyotekelezeka.
Comments are closed.