Siku 5 zaongezwa kuomba ajira Polisi

DODOMA; WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeongeza siku tano kwa watu kuomba ajira kwenye Jeshi la Polisi baada ya kuwepo tatizo la mtandao.

Tatizo la mtandao wa intaneti lilitarajiwa kuisha jana mchana. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Masauni alisema siku hizo tano zinaanza kuhesabika kesho baada ya kumalizika kwa muda
wa awali wa kuomba kujiunga na jeshi hilo la polisi kuwa leo.

Jeshi la Polisi lilitangaza Watanzania kuomba ajira kwenye jeshi hilo Mei 9, mwaka huu na mwisho wa kuwasilisha maombi hayo ikiwa ni leo.

Advertisement

Walitakiwa kutuma maombi yao kwenye Mfumo wa Ajira wa Polisi. Masauni alibainisha hayo jana bungeni wakati akijibu mwongozo ulioombwa na Mbunge wa Makete, Festus Sanga (CCM) aliyesema:

“Utaratibu wa kujiunga na polisi umetaka waombaji waandike barua na wawasilishe maombi yao kupitia Mfumo wa Ajira ya Portal ya Polisi”. “Ukienda kwenye mfumo huu kwa kipindi hiki ambapo Afrika Mashariki inapitia changamoto ya mtandao, vijana hawa wapo nje wanahangaika namna ya kupata tovuti hii ili waombe ajira hizo”.

“Pia portal (mfumo wa ajira) imezidiwa, vijana wengi hawawezi kuingia ama uwezo ni mdogo au jinsi gani mfumo haufanyi kazi vizuri. Naomba mwongozo mwenyekiti (Deo Mwanyika). Vijana wana ‘presha’ na taifa limepitia mtikisiko, jambo hili lina maslahi makubwa kwa vijana wa Tanzania”.

Kutokana na mwongozo huo, Mwenyekiti wa Bunge, Mwanyika akampa nafasi Masauni atolee kauli ya serikali ambaye alisema: “Sisi serikali tulishaliona hili na mimi na wenzangu wa timu ya wizara na Jeshi la Polisi jana (juzi) tulikaa tukajadili hili na tukaamua tuongeze siku tano baada ya deadline (mwisho wa maombi)”.

Naye Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye alitoa maelezo: “Nipongeze uamuzi wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuongeza siku ni jambo la kiungwana. Hivi tunavyoongea zaidi ya asilimia 80 ya mtandao umesharudi hali yake na nina hakika ikifika mchana (jana) tutakuwa katika mazingira mazuri”