SIKU YA JUMUIYA YA AFRIKA MASHARIKI: Manufaa yake makubwa kisiasa, kiuchumi yatajwa

WAKATI kesho ni Siku ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya hiyo imeelezwa kuwa na manufaa makubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii kwa nchi wanachama kuliko ilivyokuwa kabla ya kuanzishwa tena Novemba 30, 1999.

Wanaharakati na watetezi wa haki za binadamu na wachambuzi wa masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii, walisema hayo jana walipozungumza na HabariLEO Afrika Mashariki kuhusu maadhimisho ya siku hiyo.

Wamesema EAC imechangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha amani, kupunguza migogoro na kutafuta njia mbalimbali kumaliza migogoro miongoni mwa nchi wanachama kama inavyofanya sasa kushughulikia mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Gabriel Mwang’onda ambaye ni mchambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, alisema kuongezeka kwa nchi wanachama wa EAC kutoka tatu za Tanzania, Uganda na Kenya jumuiya hiyo ilipoanzishwa tena mwaka 1999 hadi kufikia nchi saba sasa, kumepanua soko la kanda hiyo kutoka watu milioni 120 hadi kufikia zaidi ya milioni 200.

Alisema ongezeko hilo limewezesha na kurahisisha uwezekano wa kusaidiana wakati wa hali ngumu. Alitoa mfano wa mataifa ya Burundi, Sudan Kusini na DRC, ni miongoni mwa mataifa yaliyofaidika kwa kupata msaada katika kukabiliana na migogoro ya ndani ya nchi.

“Kwa upande wa kijamii ushirikiano wa nchi saba za Afrika Mashariki umewezesha mataifa wanachama kushirikiana katika michezo mbalimbali kama ya wabunge inayoendelea sasa huko Juba nchini Sudan Kusini katika michuano ya majeshi ya Afrika Mashariki,” alisema Mwang’onda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema ongezeko la nchi kutoka tatu hadi saba katika EAC limesaidia kuimarisha uhusiano kati ya nchi na nchi wanachama. Alitoa mfano wa Burundi kabla ya kujiunga na EAC ilifikiriwa kama nchi ya vita pamoja na Sudan Kusini.

Alisema EAC imesaidia wananchi wa nchi wanachama kupata haki ingawa si moja kwa moja kupitia Mahakama ya Afrika Mashariki (EACJ) kwa kushughulikia na kutoa uamuzi kuhusu malalamiko dhidi ya serikali na taasisi mbalimbali katika nchi zao.

Kuwepo kwa nchi saba zikiwa katika hali tofauti kumesaidia nchi zenye matatizo kama ya ukabila na migogoro kujifunza na kuiga nchi zenye amani na kutokuwa na ukabila kama Tanzania kutokana na mfano bora kwao ambao umesaidia kubadili mwelekeo,” alisema Henga.

Kwa mujibu wa tangazo la Sekretarieti ya EAC, shughuli zitakazofanyika katika maadhimisho hayo ni usafishaji mazingira zitakazofanywa na wafanyakazi wa EAC katika Soko la Kilombero, upandaji miti katika Hospitali ya Levolosi na uchangiaji wa vifaa vya kujifungulia katika Hospitali ya Levolosi zote jijini Arusha, na maonesho ya wachuuzi katika Makao Makuu ya EAC yaliyopo Arusha.

Madhumuni ya jumla ya kuadhimisha siku hii ni kutoa fursa kwa EAC kutafakari dira ya mtangamano na kusherehekea maendeleo yaliyofikiwa katika mihimili ya mtangamano ambayo ni umoja wa forodha, soko la pamoja, umoja wa fedha na shirikisho la kisiasa.

Malengo mahususi yametajwa kuwa ni kutangaza siku hiyo kwa umma kwa kuwapa wananchi maarifa ya pamoja kuhusu mchakato wa mtangamano, kujadili hali ya mchakato wa ujumuishaji na kuongeza uelewa wa miradi na programu za EAC kwa umma.

Miongoni mwa matukio yatakayofanyika kesho pia ni kufanya shughuli za uwajibikaji kwa umma na shughuli za kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mkataba wa kuanzishwa kwa EAC ulitiwa saini Novemba 30, 1999 na kuanza kutumika Julai 7, 2000 baada ya kuridhiwa na nchi tatu washirika wa awali ambazo ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Kwa sasa nchi nyingine wanachama wa EAC ni Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na DRC iliyojiunga mwaka huu.

Habari Zifananazo

Back to top button