- Matumizi ya tumbaku, starehe yenye gharama
MATUMIZI ya tumbaku yanatajwa kuwa miongoni mwa matishio makubwa ya afya ya umma. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tumbaku huua takribani nusu ya watu wanaoitumia.
Zao la tumbaku ni kati ya mazao yanayoingizia nchi ya Tanzania fedha nyingi katika pato la taifa lakini ni hatari. Watanzania zaidi ya 17,200 hufa kwa magonjwa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku kila mwaka.
WHO pia inasema uvutaji wa sigara miongoni mwa wanawake unaongezeka duniani kote wakati kampuni za sigara zikiwalenga wanawake katika kampeni zake za kutafuta masoko.
Wakati leo ikiadhimishwa siku ya kupinga matumizi ya tumbaku duniani, WHO inasema miongoni mwa watu milioni tano wanaokufa kila mwaka kutokana na athari za tumbaku, milioni 1.5 ni wanawake.
Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku huadhimishwa kila mwaka tarehe 31 Mei na mwaka huu Shirika la Afya Duniani linawalenga wasichana na wanawake na kutoa wito wa juhudi zaidi za serikali kuwalinda kutokana na uvutaji wa sigara na kushiriki biashara ya kutangaza tumbaku.
Shirika hilo linasema kampuni za tumbaku zinawalenga wanawake na wasichana katika juhudi za kuchukua nafasi ya wanaoacha kuvuta au wanaokufa mapema kutokana na maradhi yanayochangiwa na bidhaa za tumbaku.
Limeongeza kuwa kampuni za tumbaku zinawafanya wanawake waamini kuwa uvutaji sigara ni ishara ya kustaarabika na inawasaidia kupunguza unene.
Shirika hilo linasema wanawake wanaovuta sigara wako katika hatari ya kutokuzaa, kuzaa kabla ya siku na ongezeko la kupata saratani ya kizazi.
Dk Kerstin Schotte, Ofisa wa kiufundi kitengo cha kuzuia magonjwa yasiyo ya kuambukizwa, NCDs, anasema kuna hatua ambazo nchi zinaweza kuchukua ili kupunguza matumizi ya tumbaku ikiwemo kutokomeza aina zote za matangazo ya tumbaku na kampeni na kutoa taarifa kwa umma kuhusu hatari za kuvuta tumbaku.
Sote tunajua kwamba uvutaji wa tumbaku ni hatari lakini cha kushangaza utafiti wa kukabiliana na matumizi ya tumbaku unaonesha kwamba watu wengi hawafahamu athari za tumbaku.
Kuongeza bei ya bidhaa za tumbaku kutapunguza matumizi hususani miongoni mwa vijana kwani vijana hawataanza matumizi ya tumbaku iwapo hawataweza kugharamia na watumiaji wa tumbaku watapunguza matumizi ya bidhaa hizo.”
Vilevile Shirika la Afya linasema linategemea ushirikiano wa nchi wanachama kuweka mikakati hiyo kwa ajili ya kukabiliana na matumizi ya tumbaku.
Wakati tukiadhimisha siku hii Shirika la Afya Duniani linatoa ujumbe wake kwa kuangazia madhara ya matumizi ya tumbaku katika mapafu ya binadamu na kuelekeza zaidi kwamba zaidi ya asilimia 40 ya vifo vinavyotokea vinatokana na utumiaji wa tumbaku ambapo ni kuhusiana na magonjwa kama saratani, magonjwa sugu ya njia ya hewa na Kifua Kikuu.
Ni kwa mantiki hiyo mwaka huu Shirika la Afya Duniani linataka serikali na wadau ziongeze hatua za kulinda watu dhidi ya tumbaku.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani, Dk Tedros Ghebreyesus anafafanua kwa kina juu ya madhara ya matumizi ya tumbaku, anasema: “Kila mwaka watu wapatao milioni 8 hufariki dunia kutokana na tumbaku. Mamilioni ya wengine wanaishi na magonjwa sugu kama vile saratani, Kifua Kikuu, pumu au magonjwa sugu ya njia ya hewa yanayosababishwa na matumizi ya tumbaku.”
Aidha, Dk Ghebreyesus anasema, “mapafu yenye afya ni muhimu kwa mtu kuishi maisha yenye afya. Leo na kila siku unaweza kulinda mapafu yako na yale ya rafiki zako na familia yako kwa kukataa kutumia tumbaku.
”
Hata hivyo, Shirika la Afya Duniani linasema matumizi ya tumbaku hayajaacha watoto salama kwa kuwa, zaidi ya watoto 60,000 wenye umri wa chini ya miaka 5 hufariki dunia kutokana na kuvuta moshi watu wavutao sigara.
Na wale wanaoishi hadi kufikia utu uzima wako kwenye nafasi kubwa zaidi ya kupata magonjwa sugu ya njia ya hewa pindi wanapokuwa wakubwa.
Mvuto mmoja tu wa moshi wa sigara una mamia ya kemikali za sumu ambazo uharibu mapafu.
Katika kufafanua zaidi juu ya jinsi gani moshi wa sigara huharibu mapafu, Shirika la Afya Duniani linasema kwamba mvuto mmoja tu wa moshi wa sigara una mamia ya kemikali za sumu ambazo huanza kuharibu mapafu.
Hii ni kwa sababu pindi moshi unapovutwa, mifumo ya kusafisha makohozi na uchafu kutoka kwenye mapafu inadhoofishwa na hivyo kuruhusu sumu iliyomo kwenye tumbaku kuingia kwenye mapafu kwa urahisi.
Shirika la Afya linasema kuwa matokeo yake, uwezo wa mapafu kufanya kazi unapungua na mvutaji anaanza kukosa pumzi na hivyo kusababisha njia za hewa kuanza kuvimba na kujenga makohozi, ‘na hivi ndivyo ambavyo tumbaku huanza kuharibu mapafu.’
Na kuhusu nini cha kufanya, Shirika la Afya linasisitiza serikali zitokomeze janga la tumbaku kwa kutekeleza kwa kina mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumzi ya tumbaku, FCTC na kuimarisha hatua dhidi ya matumizi ya tumbaku.
Hatua hizo ni pamoja na kupunguza matumizi ya tumbaku kwa kuongeza kodi ya bidhaa hizo, kutenga maeneo ambayo kwamo mtu haruhusiwi kuvuta sigara na kusaidia wale ambao wanataka kuondokana na uvutaji wa sigara.
Na kwa ngazi ya familia, Shirika la Afya linasihi wazazi na viongozi wa kijamii kuchukua hatua kulinda afya za wanafamilia kwa kuwaeleza kinagaubaga madhara ya matumizi ya tumbaku na mbinu za kujiepusha na matumizi.
Halikadhalika Shirika la Afya linasisitiza kuwa udhibiti wa tumbaku utasaidia kufanikisha kupunguza kwa theluthi moja ifikapo mwaka 2030 idadi ya watu wanaofariki dunia kabla ya muda wao kutokana na kuvuta tumbaku na kwamba kwa hali ilivyo sasa bado dunia haiko kwenye mwelekeo wa kutimiza lengo hilo.
Inasemwa kuwa gharama za magonjwa yatokanayo na matumizi ya tumbaku kila mwaka ni dola trilioni 1.4 kote duniani. Shirika la Afya linasema gharama hii ni kubwa lakini faida za kuacha uvutaji wa tumbaku kwa asilimia 20 ya watu duniani kote ambao wanatumia bidhaa hii ni kubwa zaidi, huku mapafu ya mvutaji tumbaku yakirekebika katika muda wa wiki mbili tu.
Shirika hilo linaongeza kuwa safari ni ndefu katika kutokomeza matumizi ya tumbaku kwani kufikia sasa ni asilimia 20 tu ya nchi ndizo zimefikia malengo ya kupunguza matumizi ya tumbaku.
Aidha, katika uchunguzi zaidi unaonesha kuwa kuna ongezeko kubwa zaidi la vijana wenye tabia ya kuvuta na kati ya vijana wenye umri chini ya miaka 20 wenye asilimia kubwa ya uvutaji.
Hii ni kwa mujibu wa ripoti kuhusu uvutaji iliyowasilishwa katika Taasisi Kuu ya Afya katika fursa hii ya Siku ya kupinga matumizi ya tumbaku 2023.
Kwa hakika ni siku ya kutafakari kwa pamoja duniani kuhusu hatari zinazohusiana na moshi wa tumbaku.
0685 666964 au bjhiluka@yahoo.com