SIKU YA KUPINGA MATUMIZI YA DAWA ZA KULEVYA DUNIANI
- Takwimu sahihi msaada kutambua mwenendo biashara ya mihadarati
TANGU mwaka 1989, Jumuiya ya Kimataifa imekuwa ikiadhimisha Siku ya Kupambana na Biashara na Matumizi Haramu ya Dawa za Kulevya Duniani kila tarehe 26 Juni.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa (UN) inayohusika na Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) inasema, lengo ni kusaidia maboresho ya uelewa mpana zaidi wa mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya duniani.
Matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake ni kikwazo kwa maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu.
Kwa kutambua umuhimu wa vita hiyo, UN inasema, kuwasikiliza watoto na vijana ni hatua ya kwanza ya kupambana na hali hii ambayo imeendelea kuwasumbua vijana wengi duniani.
Lengo la siku hii ni kushughulikia changamoto za dawa za kulevya katika majanga ya kiafya na kibinadamu.
Kuhakikisha upatikanaji wa dawa zinazodhibitiwa, uhakikisho wa utunzaji unaotegemea ushahidi, matibabu na huduma, na kuzuia tabia mbaya za kukabiliana na hali kupitia usaidizi ni miongoni mwa miito ya kuchukua hatua iliyoangaziwa siku hiyo na katika ofisi ya UNODC.
Kama ripoti mpya ya dunia ya dawa za kulevya inavyoeleza, nchi za Afrika Magharibi na Kati zimeathiriwa sana na tatizo la dawa za kulevya, licha ya kwamba kwa muda mrefu zimekuwa kama eneo la kupita tu.
“Katika muktadha wa majanga ya kiafya na kibinadamu, Afrika Magharibi na Kati lazima iendelee kuwekeza katika ukusanyaji na uchambuzi wa data, ikigawanywa kwa jinsia na umri, ili kuimarisha maonyo ya mapema na majibu ya msingi,” anasema Dk Amado de Andres, Mkurugenzi wa UNODC.
Ripoti ya UNODC inaonesha vifo vitokanavyo na matumizi ya dawa za kulevya vimeongezeka katika muongo uliopita.
Maambukizi mapya ya virusi vya Ukimwi (VVU) kwa watu wazima duniani kote yamepungua kwa miaka ya hivi karibuni, lakini si kwa watu wanaojichoma dawa za kulevya, ambao wanafikia asilimia 10 ya waathirika wapya.
Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, anasema ingawa nchi zinashirikiana kudhibiti usafirishaji haramu wa dawa za kulevya lakini nchi nyingi zenye kipato cha chini zina mifumo dhaifu ambayo inaruhusu biashara hiyo kuendelea.
“Kuna utofauti mkubwa kwenye nchi zenye kipato cha chini na cha kati katika suala la upatikanaji wa dawa muhimu zinazodhibitiwa. Kwa mfano, wataalamu wa matibabu Afrika Magharibi na Kati wanatoa dozi nne za dawa za maumivu kila siku kwa wakazi milioni moja, wakati Amerika ya Kaskazini idadi ya vipimo ni karibu 32,000.
Anashauri vyombo vya ulinzi na usalama kuwasaka wahusika wakuu wa usafirishaji wa dawa za kulevya badala ya kuwakamata tu watumiaji iwapo wanataka kumaliza tatizo katika nchi zao.
Anazihimiza nchi wanachama kutumia takwimu kutafuta suluhu, kwani uwepo wa takwimu bora utasaidia kutambua mwenendo na kuwezesha ufuatiliaji wa wakati halisi wa njia za usafirishaji zinazohama haraka.
Pia mifumo ya kutoa tahadhari mapema ya kisayansi itasaidia kutabiri vitisho vitakavyoibuka vya dawa za kulevya.
UN inabainisha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni vitendo vyenye madhara makubwa kwa ustawi wa jamii.
Huu ni uhalifu kama ilivyo uhalifu mwingine unaotokana na biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu na kadhalika.
Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sheria wa kitaifa na kimataifa!
Waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.
Matumizi haramu ya dawa za kulevya yana madhara makubwa kwa afya, maisha na jamii katika ujumla wake hivyo lazima watu wote wapambane nayo.
Ni dhamana kwa serikali kuhakikisha zinapambana kufa na kupona na biashara hii haramu kwa kuwashughulikia kisheria wote wanaoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo miongoni mwa vijana!
Matumizi haramu ya dawa za kulevya kwa njia ya mitandao ni hatari inayoendelea kujionesha kila kukicha na vijana ndio wanaotumbukizwa kwa urahisi katika janga hilo na kupoteza maana ya maisha.
Serikali na taasisi za dini zinapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu na mahitaji yake msingi apewe kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya kiuchumi, kijamii na kitamaduni.
Katika ulimwengu wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, taasisi za dini zinatakiwa kumweka binadamu kiini cha sera na mikakati yake ya shughuli za kiimani.
Zinapaswa zishirikiane na kushikamana na serikali na wadau sehemu mbalimbali kuelimisha, kuzuia, kurekebisha na kuwaponya waathirika wa dawa za kulevya, ili kuwarejeshea tena utu na heshima yao kama binadamu.
Pia viongozi wa vyama vya siasa wanatakiwa kutumia majukwaa yao kukemea biashara na matumizi ya dawa za kulevya.
Wanasiasa hawana budi kutumia vikao mbalimbali na mikutano ya hadhara kuunga mkono serikali katika mapambano haya.
Kwa Tanzania, maadhimisho haya yamefanyika jana, Juni 25, jijini Arusha.
Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo anabainisha lengo la siku hii ni kuongeza uelewa wa jamii na kuhamasisha umma kushiriki katika mapambano hayo.
Anasema pamoja na kwamba maadhimisho hayo duniani hufanyika Juni 26, Tanzania kwa mwaka huu kitaifa ni kuanzia Juni 23 hadi Juni 25 jijini Arusha.
Maadhimisho haya yameambatana na maonesho ya shughuli za udhibiti zinazofanywa na mamlaka hiyo pamoja na wadau wake katika udhibiti wa dawa za kulevya na utoaji elimu.
0755 666964 au bjhiluka@yahoo.com