‘Siku ya Mkulima Shambani itumike kubadilishana uzoefu’ 

WAKULIMA nchini wametakiwa kuitumia Siku ya Mkulima Shambani kujifunza fursa mbalimbali pamoja na kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu bora za kilimo.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mkulima Shambani yaliyoandaliwa na kampuni binafsi ya mbegu bora za kilimo nchini, yaliyofanyika katika mashamba ya mfano ya karanga katika vijiji vya Nguji, Mundemu na Mkondai katika Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma.

Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Alssem, Dk Emmanuel Monyo amewataka wakulima nchini kuitumia siku ya mkulima kujifunza fursa mbalimbali pamoja na kubadilishana uzoefu sambamba na kujifunza mbinu bora za kilimo.

Advertisement

Dk Monyo alisema wakiwa kama wadau wanaohusika na masuala ya mbegu ambao wanamiliki kampuni binafsi, wanapenda kufanya kazi na wakulima kwa lengo la kuwafundisha namna bora ya kuzalisha mbegu bora ili waweze kuzinunua na kuzisambaza.

Kwa upande wake, Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) Naliendele, Gerald Alex alisema katika kusherehekea siku ya mkulima shambani wameshirikiana na wadau mbalimbali kama kampuni za kuzalisha mbegu kama Alssem, Shirika la Dodoma Agriculture Seeds Production Association (Daspa) pamoja na vikundi vya wakulima.

Alisema upatikanaji wa mbegu upo kwa uhakika kama watafiti wataendelea kuzalisha mbegu za kutosha ili kampuni ziweze kupata mbegu hizo ambazo watazizalisha kuwafikia wakulima wengi na zaidi hasa Wilaya ya Bahi.

“Kwa awamu ya kwanza katika wilaya hii, tumeweza kuwafikia wakulima zaidi ya 20. Tunaamini wakulima hao watazizalisha mbegu kwa wilaya nzima.

“Tukiunganisha na vikundi walivyoungana, tuna uhakika upatikanaji wa mbegu katika wilaya hii utakuwa wa kutosha.

“Watu watapata mbegu kwa bei rahisi na upatikanaji wake utakuwa rahisi,” alisema.

Mwakilishi wa Alssem katika Wilaya ya Bahi, Anton Sahali alisema kazi kubwa wanayofanya wilayani hapo ni kuwahamasisha wakulima kulima zao la karanga.