SIKU YA WAATHIRIKA WA AJALI BARABARANI

  • Tufanye haya kuzuia majanga ya ajali za barabarani

NOVEMBA 20, ilikuwa Siku ya Kimataifa ya Kumbukumbu ya Waathirika wa Ajali za Barabarani, ambapo kwa hapa Tanzania, Asasi ya Mabalozi wa Usalama Barabarani (RSA), waliadhimisha siku hiyo kwa kutembelea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kutoa misaada ya vitu  likiwa kama tukio pekee la kitaifa la kuadhimisha siku hiyo.

Kihistoria siku hii iliasisiwa na shirika lisilo la kiserikali la Road Peace la Uingereza mwaka 1993 na miaka 12 baadaye, mwaka 2005, Umoja wa Mataifa (UN), ukaitambua, kuirasimisha na kuijumuisha kwenye kalenda ya matukio ya mwaka ya umoja huo.

Tangu wakati huo, nchi wanachama wa UN zikaanza kuitambua licha ya kwamba mataifa mengi bado hayafanyi maadhimisho haya kwa uzito unaoendana na ukubwa wa tatizo na madhara ya ajali za barabarani kiuchumi na kijamii.

Ujumbe mahususi wa maadhimisho ya mwaka huu ulikuwa “Kumbuka, Saidia, Chukua Hatua” ukilenga kuhamasisha jamii kuongeza nguvu katika kushughulikia janga hili ambalo linaendelea kukua kwa kadiri dunia inavyozidi kuendelea.

Kwa hapa nyumbani, utamaduni wa kuwakumbuka wapendwa wetu waliotangulia mbele za haki, tumekuwa nao kutokana na misingi ama ya kiimani au kimila, hivyo ni eneo ambalo ni sahihi kusema tuko vizuri. Licha ya kuwa hatufanyi hivyo kwa kuwalenga waathirika wa ajali peke yao. Maeneo mawili yaliyosalia ya ujumbe huo, (saidia na chukua hatua) ndiyo ambayo hatujawa vizuri.

Je, ni kwanini tunapaswa kusaidia waathirika wa ajali za barabarani?

Kwa mtu ambaye hajawahi kupata ajali ya barabarani, ni rahisi kudhani kuwa madhara ya matukio haya hayamuathiri na hivyo kutoona umuhimu wa yeye kutoa msaada kwa wale ambao yamewakumba. Lakini ukweli ni kwamba, madhara ya matukio hayo huathiri waliopata ajali na wasiopata ajali.

Ajali za barabarani zimekuwa zikichangia uhaba wa baadhi ya huduma muhimu za afya mfano upatikanaji wa damu. Hospitali nyingi nchini zimekuwa zikitumia kiasi kikubwa cha damu kinachochangishwa kutoka kwa wasamaria wanaojitolea, katika kuhudumia wagonjwa wa ajali za barabarani jambo ambalo limekuwa likisababisha wagonjwa wengine kukosa huduma hizo.

Unapodhani kuwa ajali ya barabarani haikuathiri kwa sababu hukuhusika, ni vyema kufahamu kuwa unaweza kuwa na mjamzito mathalani ambaye anaweza kwenda hospitali na akakosa msaada wa damu kwa kuwa iliyokuwepo imetolewa kwa wagonjwa wa ajali. Au unaweza kuwa na mtoto au mzazi anahitaji kufanyiwa upasuaji lakini akakosa huduma hiyo ya damu kutokana na sababu hiyo hiyo.

Hivyo, Watanzania tunapaswa kubadili fikra zetu sasa na kufahamu kuwa ajali zinatuathiri sote na hivyo sote tunao wajibu wa kutoa misaada kwa waathirika wa matukio hayo na uzoefu unaonesha kuwa msaada mkubwa tunaoweza kuutoa ni kwa sisi kujitokeza kwa wingi kujitolea damu ili kuziwezesha hospitali zetu kutoa matibabu kwa wepesi zaidi.

Wapo watoto ambao wamepoteza wazazi wao kwenye ajali. Hili ni kundi ambalo lilikuwa na ndoto nyingi, ambalo tunapaswa kulisaidia ili wafikie ndoto zao kimasomo na hivyo kupunguza wimbi la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi.

Je, ni hatua zipi tunapaswa kuchukua?

Kupitia maadhimisho ya siku ya waathirika wa ajali za barabarani duniani, tunakumbushwa pia juu ya kuchukua hatua kupunguza madhara ya ajali za barabarani, miongoni mwa hizo ni kuimarisha na kuboresha upatikanaji wa huduma za dharura na haraka zinazohitajika baada ya tukio la ajali.

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), idadi ya watu ambao wanaopata madhara kama kupoteza maisha au kupata ulemavu kutokana na kukosekana kwa huduma za haraka na zinazostahili katika eneo ajali ilipotokea ni kubwa.

Hivyo serikali kwa kushirikiana na wananchi tunao wajibu mkubwa wa kupanga mikakati ya kuhakikisha kuwa jambo hili linafanyiwa kazi kwa haraka iwezekanavyo.

Aidha, kuna taarifa nyingi kuhusu waathirika wa ajali za barabarani kushindwa kumudu gharama za matibabu na hivyo kupoteza maisha au kuishia kupata ulemavu wa kudumu, jambo ambalo lingeweza kuepushwa endapo wahusika wangeweza kuhudumiwa na kampuni za bima ambako vyombo vilivyopata ajali vililipia huduma hizo.

Sheria, kanuni na taratibu zetu za bima kwa sasa zina mlolongo mrefu na urasimu mwingi wakati mwingine hivyo kuwakosesha waathirika haki ya kupata fidia wanazostahili na hili likimaanisha ipo haja sasa ya wadau wa sekta ya bima kwa kushirikiana na mamlaka kuangalia upya taratibu za ulipaji fidia zinazohusiana na ajali za barabarani.

Hatua nyingine ya kuchukuliwa ni kwa serikali yetu kuharakisha upatikanaji wa sheria mpya ya usalama barabarani. Tunatambua muswada wa mabadiliko yake ulisomwa bungeni mwaka 2020, baada ya hapo muswada huo ukakwama tena, hivyo Waziri mwenye dhamana ya kushughulikia muswada huo tunaomba achagize kuhuisha mchakato wake ili tupate sheria itakayonusuru Watanzania dhidi ya ajali.

Nihitimishe makala haya kwa kulitaja eneo muhimu zaidi ambalo tunapaswa kuchukua hatua, ambalo ni eneo la uelimishaji. Tafiti zinaonesha kuwa, majanga mengi ya ajali za barabarani yanatokana na watumia barabara kutokuwa na elimu ya usalama barabarani, hivyo jamii inapaswa kuongeza nguvu kubwa zaidi katika kuhakikisha tunakuwa na mfumo mzuri wa utoaji elimu ya matumizi sahihi na salama ya barabara kwa watumiaji wa makundi yote.

Ajali za barabarani zinaua wapendwa wetu, zinaua ndoto zetu, zinadumaza ustawi wa uchumi wa jamii na taifa kwa ujumla, ajali zinasambaratisha familia, ndoa kuvunjika na ongezeko la watoto wanaoishi kwenye mazingira hatarishi. Hakuna awezaye kuwa salama barabarani ikiwa mwenzake hayuko salama. Kama ambavyo janga la ajali ni letu sote, ndivyo ambavyo usalama barabarani ni jukumu letu sote.

Mwandishi wa makala haya ni Balozi wa Usalama Barabarani (RSA). Mawasiliano 0713412176, msangirs@gmail.com

 

Habari Zifananazo

Back to top button