Silinde atoa maagizo kwa wakandarasi wa miradi umwagiliaji

SIMIYU:NAIBU Waziri wa Kilimo, David Silinde amewataka wakandarasi wa miradi yote ya umwagiliaji nchini kuwajibika kwa kutoa taarifa ya utekelezaji wa miradi yao katika maeneo waliyopo, ili kujenga mahusiano mazuri kati yao na Serikali za Wilaya au Mikoa.

Silinde amesema hayo alipotembelea ujenzi wa bwawa la Kasoli, Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi katika kukagua shughuli mbalimbali za kilimo na zile zinazoratibiwa na bodi ya pamba, katika Mkoa wa Simiyu.

Wakandarasi wameaswa kuzingatia maelekezo wanayopewa pindi wanapopata kazi za miradi na kutoa taarifa za utekelezaji wao kwenye ofisi za serikali za maeneo husika kuanzia ngazi za kijiji hadi mkoa.

Aidha, Silinde amesema kuwa Tume ya Umwagiliaji iliyo chini ya Wizara ya Kilimo imepanga mwaka huu wa fedha kufanya ujenzi mpya wa mabwawa 100 nchi nzima ili kumsaidia mkulima kuweza kulima mwaka mzima bila kutegemea mvua.

Ametoa rai kuwa wananchi wapatiwe elimu kuhusu umuhimu wa miradi ya umwagiliaji na utunzaji wa miundombinu yake kwani watakaonufaika ni wao hivyo wanapaswa kuwa walinzi namba moja wa miradi hiyo.

Mradi wa ujenzi wa bwawa la Kasoli ni wa gharama ya Sh bilioni 8 na unatakiwa kuwa umekamilika ifikapo mwezi Julai 2024.  Hadi sasa ujenzi umefiakia asilimia 40 na kukamilika kwake kutawanufaisha wakulima zaidi ya 720 ili kuongeza tija ya uzalishaji wa mahindi na mpunga.

Habari Zifananazo

Back to top button