ZANZIBAR; BAO la kiungo Msenegal Babacar Sarr dakika ya 77, limeiwezesha Simba kuibuka bingwa mpya wa michuano ya Kombe la Muungano kwa ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa fainali dhidi ya Azam Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Ni ushindi ambao umeibua shangwe kwa wachezaji, viongozi wadau na mashabiki wa Simba kwa kutwaa ubingwa wa michuano hiyo iliyorejeshwa tena baada ya kusimama kwa zaidi ya miaka 20.
Kutokana na ubingwa huo ambao Simba walikabidhiwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, Simba imezawadiwa pia Sh milioni 50, wakati Azam iliyoshika nafasi ya pili ikivuna Sh milioni 30.
Sarr amefunga bao hilo akiunganisha kwa kichwa mpira wa adhabu uliopigwa na Israel Mwenda, adhabu iliyotokana na kiungo mshambuliaji Willy Onana kuangushwa nje kidogo ya eneo la boksi. Simba sasa imetwaa kombe hilo mara sita sawa na Yanga katika historia ya michuano hiyo.