Simba fungu la kukosa
MWAKA 2023 umeendelea kuwa mgumu kwa timu ya Simba baada ya jana kuondoshwa kwenye hatua ya nusu fainali ya kombe la shirikisho la Azam na timu ya Azam kwa kufungwa mabao 2-1 Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Wekundu hao wa Msimbazi waliondoshwa kwenye hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Wydad Casablanca kwa mikwaju ya penalti 4-3 Uwanja wa Mohamedi V Morocco baada ya wenyeji kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dakika 90 za mchezo huo. Mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Simba ilishinda bao 1-0.
Baada ya wiki iliyopita kutoka sare ya bao 1-1 na Namungo, matumiani pekee ya timu hiyo walau kuambulia chochote yalibaki kwenye michuano ya kombe la Shirikisho la Azam(FA) kwani wapinzani wao wakubwa Yanga wanahitaji kushinda mechi moja tu kati ya mitatu iliyosalia kutetea ubingwa wa Ligi Kuu.
Katika mchezo wa jana Azam walitangulia kwa bao la beki Lusajo Mwaikenda dakika ya 22 na Simba kusawazisha kupitia kwa Sadio Kanoute dakika ya 27 na Prince Dube kuifungia Azam bao la ushindi dakika ya 75 na kuondoa matumaini ya Simba ya walau kunyakua taji lolote msimu huu.
Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko zilikuwa sare ya bao 1-1 huku mchezo ukionekana kubalansi kwa timu zote kushambuliana kwa zamu.
Kipindi cha pili Simba walikianza kwa kasi na kufanya mashambulizi mengi lakini washambuliaji wa Simba, Clatous Chama na Jean Baleke walikosa utulivu baada ya kushindwa kuzitumia vyema nafasi walizozipata.
Dube aliyengia dakika ya 66 kuchukua nafasi ya Idriss Mbombo aliifungia Azam bao la ushindi na la tatu kwa msimu huu dhidi ya Simba huku wekundu hao wa Msimbazi wakipata pigo kwa kiungo wake Kanoute kuoneshwa kadi nyekundu dakika ya 87 kwa kumfanyia madhambi James Akaminko wa Azam akiwa tayari ameshachezea kadi ya njano.
Azam sasa itasubiri mshindi kati ya Yanga na Singida Big Stars kucheza naye fainali za mashindano hayo mwishoni mwa mwezi huu.