Simba hasira zote kwa Namungo leo

SIMBA imeeleza kuwa iko tayari na imejiandaa vya kutosha kuumana na Namungo leo ikiwa wameelekeza nguvu zao zote kwenye Ligi Kuu Bara na Kombe la FA (ASFC) kwa sasa.

Hayo yamesemwa na kocha msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda jana akieleza kuwa wachezaji wako tayari kwa ajili ya mchezo huo utakaopigwa Uwanja wa Majaliwa, Lindi hata kabla ya kwenda Morocco kuumana na Wydad Casablanca kwenye robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Alisema walifahamu kwamba hata iweje lazima wangecheza na Namungo hivyo walikuwa tayari kwa ajili ya hilo na sasa wamewekeza nguvu zaidi kwenye michuano ya ndani baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika na Wydad kwa penalti 4-3 wiki iliyopita.

“Hii mechi ilikuwepo kabla ya kwenda Morocco na wachezaji walilifahamu hilo, bila ya kujali matokeo kwa hiyo morali ya kucheza na Namungo iko palepale, pia jukumu lililotupeleka Morocco hatunalo tena. “Jukumu tulilonalo sasa hivi ni mechi za ligi na mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (FA), wachezaji wanatambua wajibu wao huo kwa hiyo kwa ufupi tuko tayari kuendelea na majukumu yaliyo mbele yetu,” alisema Mgunda.

Alisisitiza kuwa wanafahamu wanakutana na timu nzuri, yenye ushindani kwenye ligi na wachezaji wazoefu ndiyo maana wamejiandaa vya kutosha. Naye Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi alisema wanatambua ubora walionao Simba na nafasi waliyopo kwenye ligi, hivyo nao wamejipanga katika ubora wa juu kuweka sawa maeneo yao muhimu ili kupata matokeo.

Habari Zifananazo

1 Comment
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button