Simba kuitangaza Zanzibar

ZANZIBAR: SIMBA SC imetangaza kutumia mitandao yake ya kijamii kuutangaza utalii wa Zanzibar kwa kufanya shughuli nyingi, nje ya ushiriki wao katika michuano inayoendelea ya Kombe la Mapinduzi.

 

Mikakati hiyo imewekwa wazi leo na Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu hiyo, Iman Kajula wakati akizumgumza na waandishi wa habari visiwani Zanzibar

Advertisement

“Hii sio mara ya kwanza Simba kutangaza utalii, wote mnakumbuka kwenye CAF tulikuwa tunatangaza Visit Tanzania na sasa tunatangaza utalii wa Zanzibar kwa kuanzia kesho,” amesema Kajula.

 

Amesema kupitia mitandao yao ya kijamii yenye wingi wa wafuasi ndani bara la Afrika na maeneo mengi duniani tayari wameanza kampeni hiyo ya kutangaza kuanzia jana kupitia hashtag mbalimbali mtandaoni.

“Sisi ni maendeleo, Zanzibar inapiga hatua kubwa sana, na sisi kama klabu kubwa tumeona ni vyema kuunga mkono juhudi za serikali. Jambo hili litasaidia kukuza uchumi na watu watapata fedha ambazo watakuwa wanatumia kama mambo ya maendeleo, kununua jezi, kununua bidhaa mbalimbali za klabu na hata kuja kwenye mechi. Tutatumia siku ambazo hatuchezi mechi kutangaza maeneo ya kitalii.” Amesema CEO huyo.