SIMBA SC kesho wataingia kambini kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi watani wao Yanga SC, mchezo utakaopigwa Jumapili hii saa 11:00 uwanja wa Mkapa, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally ameeleza.
Akizungumza na waandishi wa habari Oktoba 30, 2023 Ahmed ametaja viingilio vya mchezo huo ambao Simba SC atakuwa mwenyeji. “Viingilio Mzunguko Sh 5,000, Machungwa Sh 10,000, VIP C Sh 20,000, VIP B Sh 30,000, VIP A Sh 40,000 na Platinum Sh 150,000.”
Ahmed amesema licha ya kucheza mechi kadhaa ngumu, lakini mchezo huo ni mgumu zaidi kutokana na ukubwa na hamasa ya kila timu. “Tumecheza mechi ngumu lakini mechi ya Jumapili ni ngumu kuliko zote hii ni kutokana na utani uliopo pamoja na ubora wa timu yao.”
“Ni mechi ambayo Wanasimba inabidi tujitoe muhanga ili kupata ushindi. Kila Mwanasimba ajue ana jukumu la kusaidia timu yake. Tukishinda siku hiyo shughuli itakuwa imeisha, itabaki shughuli ya kukamilisha ratiba ya msimu.”- amesema Ahmed.