ZANZIBAR: MENEJA Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally amesema katika kipindi chote cha mashindano ya Kombe la Mapinduzi watakuwa wakivaa nembo ya Zanzibar, ikiwa ni sehemu ya kutangaza utalii unaopatikana visiwani humo.
Ally ameeleza hayo leo visiwani humo, katika mkutano na waandishi wa habari kutangaza kampeni waliyoianzisha leo ya kunadi vivutio mbalimbali vinavyopatikana visiwani humo.
“Kuanzia mechi ya kesho dhidi ya Singida Fountain Gate tutavaa jezi zenye nembo ya Zanzibar. Ndani ya siku hizi 14 za kuchukua ubingwa wa Mapinduzi tutatembelea maeneo ambayo yana vivutio vizuri lakini havionekani sana, sisi tutaitangaza kupitia kurasa zetu.” amejinadi Meneja huyo.
Amesema lengo la klabu hiyo ni kuongeza namba ya watalii visiwani Zanzibar.
“Nawaomba Wanasimba tukitangaza sehemu ambayo tunatembelea mjitokeze kwa wingi.
” Amesema Ally.
Katika kutangaza utalii huo kwa njia ya mtandao, klabu hiyo imetangaza hashtag zitazotumika kuwa #UchumiWaBuluu #VisitZanzibar #WenyeNchi #NguvuMoja