KOCHA Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, ametamba kuifunga timu ya Vipers na kufufua matumaini ya timu hiyo kutinga robo fainali ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Akizungumza na HabariLEO, kocha huyo ameeleza kuwa kinachompa jeuri hiyo ni utayari kikosi cha wachezaji 24 ambao wanaondoka leo jioni kuelekea Uganda kwa ajili ya mchezo huo ambao wameupa uzito mkubwa.
“Tumejipanga kushinda mchezo dhidi ya Vipers bila kujali tupo ugenini najua haitokuwa rahisi, lakini nikwambie tu ninaimani kubwa na jeshi langu la wachezaji 24 tutafanya maajabu tukiwa ugenini,” amesema Robertinho.
Wachezaji 24 watakao safari na timu hiyo jioni ya leo ni Aishi Manula, Beno Kakolanya, Ally Salum, Shomari Kapombe, Izrael Mwenda, Mohamed Hussein, Gadiel Michael, Kennedy Juma, Mohammed Ouattara, Joashi Onyango, Henock Inonga na Erasto Nyoni.
Wengine ni Sadio Kanoute, Mzamiru Yassin,Clatous Chama, Ismail Sawadogo, Saido Ntibazonkiza, Peter Banda, Kibu Denis, Pape Sakho, John Bocco, Jean Baleke, Moses Phiri na Habibu Kyombo.
–