Simba, Mbeya City mechi ya kisasi

SIMBA leo itakuwa ugenini kumenyana na Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya katika muendelezo wa mechi za Ligi Kuu Bara.

Timu hizo zinakutana zikiwa kwenye tano bora ya msimamo wa ligi ambapo Simba ni ya tatu ikiwa na pointi 27 wakati Mbeya City ikishikilia nafasi ya tano kwa pointi 18 baada ya wote kucheza mechi 12.

Hata hivyo, Wekundu hao wanaingia katika uwanja huo wakiwa na kumbukumbu ya kufungwa bao 1-0 msimu uliopita kabla na wao kulipa kisasi cha mabao 3-0 kwenye mechi ya marudiano, hivyo mchezo huo unatarajia kuwa mgumu na wa ushindani.

Meneja wa Habari wa Mawasiliano wa Simba, Ahmed Ally alisema kuwa wako tayari kwa mchezo huo baada ya kutua juzi usiku mkoani humo ingawa watamkosa kiungo wao mkabaji, Sadio Kanoute kutokana na majeraha.

“Kikosi kipo sawa na maandalizi yako vizuri kabisa, wachezaji 22 tulionao hapa wako fiti na tayari kwa mchezo ingawa tutamkosa Kanoute ambaye aliumia mchezo wa mwisho (dhidi ya Ruvu Shooting) ambaye ripoti yake itatoka baadaye.

“Kiujumla tunafahamu mechi ni ngumu na tunajua msimu uliopita tulikosa matokeo mazuri hapa Mbeya na kuanza kuyumba juu ya kuupigania ubingwa wetu, sasa hilo tupo tayari kukabiliana nalo na vijana wapo tayari kwa ajili ya kuipambania Simba,” alisema Ally.

Kwa upande wa Mbeya City ambayo imeshinda mechi moja na kutoa sare tatu kwenye mechi nne mfululizo zilizopita katika uwanja huo, wamejinasibu kuwa wanataka kukamilisha hesabu za mechi zao tano mfululizo kwa kuibuka na ushindi dhidi ya Simba leo.

Ofisa Habari wa Mbeya, Shah Mjanja alisema benchi la ufundi lililo chini ya Abdallah Mubiru limeendelea kujipanga kwa uhakika kimbinu kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kukamilisha hesabu ya kutopoteza mchezo katika mechi hizo tano.

“Kimsingi maandalizi yako vizuri kabisa lakini kuelekea mechi yenye ushindani kama hiyo tumekuwa na maandalizi maalumu ambayo ni kwa ajili ya kuhakikisha tunakamilisha hesabu zetu vizuri.

“Tulikuwa na mechi tano mfululizo nyumbani, tumeshinda moja, sare tatu na ya mwisho ni hii ya Simba, tunahitaji ushindi hapa ili tukamilishe hesabu ya kutopoteza na kuzidi kujiweka vizuri katika msimamo,” alisema Mjanja.

Habari Zifananazo

Back to top button