Simba mdogo mdogo

Phiri alindwe kwa namna gani?

SIMBA jana imejiongezea pointi tatu muhimu baada ya kuifunga Tanzania Prisons ya Mbeya kwa bao 1-0 katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.

Hata hivyo, ushindi huo ulioifikisha pointi 10 sawa na Yanga, haujairejesha kileleni na kuiacha Yanga kushika usukani huo kwa tofauti ya mabao.

Simba wameiondoa Azam katika nafasi ya pili kwa pointi zao nane walizofikisha baada ya juzi kushinda 1-0 dhidi ya Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine.

Advertisement

Bao pekee lililoipatia pointi tatu Simba na kuwapa furaha maelfu ya mashabiki wa Simba waliohudhuria mchezo huo Uwanja wa Sokoine, lilifungwa na kiungo mkabaji, Jonas Mkude dakika ya 85 akimalizia mpira wa kichwa uliorudishwa uwanjani na Kibu Denis.

Katika mchezo huo, wenyeji Tanzania Prisons walilazimika kucheza pungufu dakika tatu za nyongeza baada ya beki wake, Jamali Masenga kutolewa nje kwa kadi nyekundu na mwamuzi Ahamed Arajiga kutoka Manyara kwa kumchezea rafu ya pili kiungo Cletus Chama.

Timu hizo ziliuanza mchezo kwa kasi ya chini katika kipindi cha kwanza na kila upande ulitengeneza nafasi kadhaa za mabao lakini washambuliaji wake hawakuwa makini katika kuzitumia. Kwa upande wa Simba, kinara wa mabao, Moses Phiri alipata nafasi kadhaa lakini mashuti mengi aliyopiga yaliishia mikononi mwa kipa wa Prisons, Hussein Abel ambaye katika kipindi hicho alifanya kazi kubwa ya kuokoa michomo mingi ya washambuliaji wa Simba.

Prisons nao walitengeneza nafasi mbili kwenye kipindi cha kwanza, lakini mshambuliaji wake, Samson Mbangula alishindwa kumalizia wavuni krosi iliyochongwa na nahodha wa timu hiyo, Jumanne El Fadhili. Kipindi cha pili Simba ilikianza kwa kuwatoa Habibu Kyombo na Hennock Inonga na nafasi zao kuchukuliwa na Kibu Denis na Joashi Onyango ambao kuingia kwao kuliongeza kasi ya mashambulizi kwenye lango la Prisons lakini safu ya ulinzi ya Prisons ilikuwa makini kuondoa hatari hizo.

Baada ya kuona mambo yanazidi kuwa magumu kocha wa muda wa Simba, Juma Mgunda alimtoa Pape Sakho na nafasi yake kumuingiza Augostino Okrah ambaye kwa kiasi kikubwa alikuwa mwiba mchungu kwa walinzi wa Prisons na ndiye aliyesababisha mpira wa adhabu ndogo iliyosababisha bao hilo pekee.

Dakika ya 61, Mbangula alikaribia kuifungia bao Prisons baada ya shuti alilopiga kugonga mwamba wa juu wa lango la Simba na mpira kurudi uwanjani na Mcha Hamis aliyeingia dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Ismail Mgunda alikosa bao baada ya kushindwa kumalizia mpira uliotokana na shambulizi la kushtukiza.