Simba Queens ina deni michuano ya CECAFA SAMIA CUP

DAR ES SALAAM katika viunga vya Chamazi inashuhudia Ligi ya Mabingwa Afrika wa Ukanda wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kwa wanawake ikitimua vumbi katika Uwanja wa Azam Complex.

Ligi hiyo ambayo inadhaminiwa na Rais Samia Suluhu Hassan inashirikisha timu nane zilizopangwa katika makundi mawili yenye timu nne kila moja na ni msimu wa pili yakifanyika na ni kwa mara ya kwanza yanafanyika nchini.

Kundi A lina timu za Commercial Bank FC ya Ethiopia inayoongoza ikifuatiwa na AS Kigali WFC ya Rwanda, Fofila PF ya Burundi na Warriors Queens ya Zanzibar na Kundi B lina vinara Simba Queens, She Corporate ya Uganda, Yei Joints Stars ya Sudan Kusini na Garde Republicane ya Djibouti.

USHINDANI

Ushindani wa msimu huu si mkubwa kama msimu uliopita, kwani hata timu zilizokuwepo msimu uliopita msimu huu zipo timu tatu, ambazo ni Simba Queens, Commercial Bank FC ya Ethiopia na Yei Joints Stars ya Sudan Kusini. Katika hizo timu zilizofika nusu fainali msimu huo ni Simba Queens na Commercial Bank ya Ethiopia ilicheza fainali na kushika nafasi ya pili pia msimu huu ndizo zinazoonesha ushindani wa kweli.

MSIMU ULIOPITA

Ligi hii kama ilivyo msimu huu inashirikisha timu nane na bingwa wa msimu uliopita Vihiga Queens ya Kenya haijashiriki kutokana na Shirikisho la Kenya (KFF) kufungiwa na Fifa baada ya serikali kuingilia masuala ya soka. Timu nyingine ambazo zilishiriki msimu uliopita na msimu huu hazipo ni mshindi wa tatu timu ya Lady Doves kutoka Uganda, PVP FC ya Burundi, FAD FC ya Djibouti na New Generation ya Zanzibar.

Kukosekana kwa Vihiga Queens na Lady Doves kumeziachia timu za Simba Queens na Commercial Bank of Ethiopia kuwa washindani ambao hata hivyo wanaweza kukutana fainali kwani kila mmoja anaongoza kundi lake na kutokana na ratiba ilivyo haziwezi kukutana katika nusu fainali. Ratiba ya nusu fainali ambayo itachezwa Agosti 24 mshindi wa kwanza wa Kundi A atacheza na mshindi wa pili wa Kundi B na mshindi wa kwanza wa Kundi B atacheza na mshindi wa pili wa Kundi A na fainali zitachezwa Agosti 27.

SIMBA QUEENS

Ikiwa ni mara yake ya pili kushiriki kama mwakilishi wa Tanzania baada ya kutwaa ubingwa wanatakiwa kupambana ili kutwaa ubingwa na kufuzu fainali baada ya kushindwa kufanya hivyo msimu uliopita na kushika nafasi ya nne.

Simba Queens inayosababu ya kutwaa ubingwa kutokana na usajili waliofanya msimu huu, kwani ina kikosi imara na cha kushindana tofauti na msimu uliopita, ambapo ilikuwa na Flavine Mawete na Danai Bhobho waliotimkia nchini Uturuki.

Hata hivyo, Simba Queens wameonesha nia ya kutwaa ubingwa kwani ilikuwa timu ya kwanza kufuzu nusu fainali kwa kuifunga She Corporate ya Uganda kwa mabao 2-0 na Garde Republicane ya Djibouti 6-0, lakini pia ina mchezo mmoja mkononi dhidi ya Yei Joints Stars.

Kocha wa Simba Queens, Sebastian Nkoma anatakiwa kuzungumza na wachezaji wake, kwani wameonekana kila mmoja anataka kufunga mwenyewe bila kuangalia kama kuna mwenzake, ambaye yupo katika nafasi nzuri zaidi yake.

Katika mchezo dhidi ya She Corporate, Asha Djafar na Oppah Clement waliikosesha timu mabao mengi tena ya wazi kwa kung’ang’ania kufunga wenyewe hivyo makosa kama hayo yanatakiwa kurekebishwa ili zile fedha zinazotolewa na Rais Samia zibaki nchini. Kwa jinsi ambavyo Simba Queens imewekeza kwa kusajili wachezaji wazuri wa ndani na wa kimataifa, wanatakiwa kufanya vizuri na hatimaye kufuzu.

ZAWADI NONO

Rais Samia amedhamini mashindano haya kwa Dola za Marekani 100,000 (sawa na Sh 233,150,000) na kufanya kuitwa Cecafa Samia Cup.

Bingwa atachukua Dola za Marekani 30,000 (sawa na Sh milioni 70), mshindi wa pili Dola 20,000 (sawa na Sh milioni 47) na mshindi wa tatu dola 10,000 (sawa na Sh milioni 23.3) pia kuna zawadi za kipa bora, mfungaji bora, mchezaji bora, kocha bora na nyingine, hivyo Simba Queens wanayosababu ya kumdhihirishia Rais Samia kuwa hakukosea kudhamini mashindano hayo na kuonesha kuwa mwaka jana waliteleza tu.

Pia watakuwa wamempa heshima Rais wa Cecafa, Wallace Karia, ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kwa ushawishi wake aliofanya kwa Rais Samia hadi akakubali kudhamini mashindano hayo.

Kazi imebaki kwa wachezaji wa Simba Queens na benchi la ufundi kuhakikisha wanaandika historia ya kuwa timu ya kwanza kufuzu hatua ya mwisho ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania mara tatu na kuwa timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo mara nyingi.

Habari Zifananazo

Back to top button