Simba v Yanga huwa ni zaidi ya mechi!

MIAMBA ya soka nchini, Simba na Yanga intarajiwa kuvaana leo katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa mwaka 2022/2023 Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kwa kawaida mechi Simba na Yanga za Dar es Salaam ni moja ya mechi zenye upinzani, msisimko na mshawasha mkubwa kupita zote katika eneo hili la Afrika Mashariki na Kati na pengine Afrika kwa ujumla wake.

Ni mechi inayokutanisha mahasimu wa jadi kwenye soka wenye tabia na tamaduni tofauti kabisa na zile ambazo wengi wamezizoea katika maisha ya soka la timu pinzani za kawaida.

Upinzani wa timu hizi ambao ulianza zaaidi ya miaka 50 iliyopita ni wa kipekee na wenye kuvutia kwa upande mmoja na upande mwingine si ya kufurahisha kabisa.

 

Kwa kawaida upinzani wa soka wa timu pinzani za kawaida unakuwepo kwa takribani zile dakika 90 pale kiwanjani na zaidi ya hapo ni maisha ya kawaida kuchukua nafasi yake.

Lakini kwa hapa kwetu mara timu hizi zinapokutana kunakuwa na uhasama kuanzia nje na wakati mwingine hadi ndani ya kiwanja.

Hali hii inafanya soka ya uhakika kukosekana pale kiwanjani kwa kile kinachoonekana wachezaji kushindwa kutulia na kutumia ufundi na ustadi wao wa kucheza kandanda kutokana na presha ya mechi yenyewe kiasili yake.

Mechi kati ya Simba na Yanga daima ni mechi inayotawaliwa na maneno yanahusu ushirikina, hujuma, fitina, rushwa na kutokuaminiana kwa kiasi kikubwa kati ya mshabiki na mshabiki, kiongozi na kiongozi, wachezaji na mashabiki, viongozi na wachezaji.

Wakati mwingine hali inakuwa mbaya kufikia hata mchezaji na mchezaji kutokuaminiana kabisa na pengine kuangushiana shutumu za aidha kutaka au kuhujumu kabisa mechi hiyo.

Hii inatokana na kile kinachoaminika kwamba mmoja kati ya pande zinazoshutumiana kuwa ni shabiki wa timu pinzani, hivyo anawewza kuwa anawahujumu wenzake kwa mantiki ya kwamba akiwa peke yake nyumbani anakuwa anafurahi kwamba timu anayoipenda kwa dhati imeshinda.

Yote haya yanatokana na ukweli kwamba nchi imegawanyika katika pande mbili tu za Simba na Yanga linapokuja suala la soka la nchi hii.

Kama kweli ni mpenzi au mshabiki wa mpira  na ushabiki au upenzi wako ulianzia hapa nchini, basi kama sio Yanga utakuwa Simba tu, hii ndo imani iliyopo.

Hali hii inaifanya mechi hii kubwa kabisa katika eneo hili la Afrika Mshariki na Kati kutokuwa ya kusisimua pale kiwanjani na badala yake mshawasha na uchangamfu wa mechi unakuwa kwa mashabiki zaidi wanaotambiana na kutukanana na hata kupigana wakati mwingine.

Wachezaji wanakuwa ni wenye presha ya hali ya juu kiasi kwamba wanajiona ni wakosaji wakati wote na kushindwa kuonesha ustadi wao wa kucheza ndinga, kwani mara unapotaka kufanya kitu cha mpira pale kiwanjani na kwa bahati mbaya ukakosea na kusababisha timu kufungwa bao, ikatokea bao hilo ndo likawapa ushindi timu pinzani, basi ujue uko kwenye matatizo makubwa.

Watu wanaweza hata kukutishia kusitisha maisha yako hapa duniani kwa kuifungisha timu yao na kuwanyima raha hapa mjini.

Ni kawaida kusikia baadhi ya wachezaji wa Simba wakishutumiwa kuwa ni wapenzi au washabiki wa Yanga na hali kadhalika ni kawaida kusikia baadhi ya wachezaji wa Yanga wakipata shutuma za wao ni Simba damu.

Huko nyuma mechi kati ya timu hizi mbili ilikuwa ni hatari ya zaidi ilivyo sasa, kwani kuna wakati kulikuwa kunachaguliwa watu wawili au watatu kutoka kila timu ili kuulinda kwa siku mbili mpira utaochezwa katika mechi hii pale makao makuu ya TFF.

Hata uingiaji wa kiwanjani wakati mwingine ulikuwa ni kwa kuruka ukuta wa pale Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru).

Hapa imani ilikuwa ni katika nyanja ya kishirikina zaidi, watu walikuwa wanaamini kwamba mpira unaweza kufanyiwa marogo ambayo yangesababisha timu yao ifungwe, na pia ukiingia kiwanjani kwa mlango wa kawaida unaweza kukanyaga ‘ulozi’ uliowekwa na mpinzani wako na kukufanya uchezee kichapo.

Kwa kiasi kikubwa mambo ya kulinda mipira na kuruka ukuta hayapo kabisa siku hizi ingawa imani za kishirikina ni vigumu kusema hakuna, hizi sina shaka zinaendelea ila katika engo tofauti na ilivyokuwa kabla.

Binafsi naona sasa wakati umefika kwa ushabiki kati ya timu hizi mbili ubadilike na uwe kimchezo zaidi hali ambayo itatoa fursa kwa wachezaji kujisikia huru na kutuonyesha ustadi wao wakiwa kiwanjani na wakikosea waishi kwa amani bila mashaka.

Kuna kazi kubwa sana inahitajika ili kusaidia kuboresha soka yetu, mbali na viongozi na wachezaji, lakini hata mashabiki pia ni tatizo kubwa katika soka ya Tanzania.

Tatizo kubwa la washabiki wa mpira hasa wale Simba na Yanga, wenyewe hawaangalii mpira , wala hawakubali uwezo wa timu pinzani zaidi ya kama ni shabiki wa Yanga, kuing’ang’ania Yanga yako na kama ni Simba kufa na Simba yako.

Shabiki wa Simba kamwe hawezi kukubali uwezo wa Yanga hata kama wamewafunga na kuwazidi kimchezo katika njia ambayo ni haki,kweli na wazi kwa kila mmoja.

Hali ni kama hiyo kwa Yanga ambao hata kama watafungwa kihalali ni kuzidiwa kwa umbali wa mbingu na ardhi, lakini hawatakaa wakubali uwezo wa Simba.

 

Zaidi ya hapo kitachofuata ni aidha mechi imeuzwa au wamenenua mechi! Wenzetu wanakubali uwezo wa timu nyingine na kuwapo changamoto wachezaji na viongozi ili kuboresha viwango vyao na kuwapa raha washabiki wao.

Mwaka 2004 kwa mra ya kwanza katika dimba l El Santiago Bernabeu pale Madrid Hispania, tmu ya Barcelona iliichapa Real Madrid ilitosheheni nyota kibao. Katika ushindi ule wa bao 3-0 walioupata Barca, mabao mawili mazuri sana yalifungwa na Ronaldinho Gaucho.

Walichokifanya mashabiki wa Bernabeu ni kusimama na kumshangilia Gaucho kwa aina ya kishujaa, hali ambayo wamekuwa wakiwapo mashujaa wao kama Zidane, Figo na Raul ambao wote walikuwepo kiwanjani wakati Gaucho anatakata na kuweka bao mbili.

Kitendo kile kiliwanyima raha nyota wa Madrid na kuomba msamaha kabla ya kuboresha kiwango chao na kushinda mechi ya marejeo.

Habari Zifananazo

Back to top button