Simba wala mifugo warejea Hifadhi ya Taifa Ruaha

BAADHI ya Simba wala mifugo waliotokea Hifadhi ya Taifa ya Ruaha na kuzua taharuki kwa wananchi mkoani Iringa kwa zaidi ya siku 20 wanadaiwa kurudi hifadhini humo.

Taarifa za Simba hao ambao kwa mara ya kwanza zilitokea katika kijiji cha Magunga wilayani Iringa kabla ya kuelekea kijiji cha Kiponzero, Tanangozi na Sadani; wanadaiwa mpaka jana kuuwa mifugo 64 zikiwemo ng’ombe 34, mbuzi, nguruwe na kuku.

Akizungumza na wanahabari leo, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Godwell Ole Meing’ataki amesema Simba hao waliokadiriwa kuwa watano, waligawanyika katika makundi mawili, moja limerudi hifadhini na lingine lipo katika kijiji cha Isingo karibu na mashamba ya mwekezaji (hakutajwa jina) ambako kuna msitu mnene.

“Tulipopata taarifa katika kuwasaka tuliweka mtego wa mbuzi na nyama katika moja ya maeneo ya msitu huo na tulipoenda kesho yake tuliona nyayo za simba huku mbuzi na nyama hiyo vikikosekana,” alisema na kuongeza kwamba matukio yote ya Simba hao kuua na kula mifugo yamekuwa yakifanyika usiku wakati wananchi wamelala.

Kuhusu Simba waliorudi hifadhini, Meing’ataki alisema taarifa zao zilipatikana katika kijiji cha Mahuninga jirani na hifadhi hiyo baada ya baadhi ya wananchi kuwaona nyakati za usiku wakipita kijijini hapo kwa kasi kuelekea hifadhini.

Akizungumzia idadi kubwa ya mifugo iliyouawa alisema hiyo ni kwasababu Simba hao walikuwa hawamalizi kumla mnyama mmoja na kushiba kwasababu ya taharuki na kelele walizokuwa wanakutana nazo kutoka kwa mifugo na wananchi.

“Kwahiyo walikuwa wanakimbia na kwenda katika maeneo mengine wakiwa na njaa na hivyo kulazimika kuvamia mazizi mengine ya watu na kukamata wanyama hao,” alisema na kuongeza kwamba kwa kawaida Simba akishiba vizuri- anawinda na kula tena baada ya siku mbili.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dedengo amewaondoa hofu wananchi hususani wa Iringa mjini akisema waendelee na shughuli zao kama kawaida kwani Simba hao hawapo katika maeneo yao kama inavyotaarifa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii.

“Kumekuwepo na taarifa za uzushi katika baadhi ya mitandao ya kijamii zinazotolewa na baadhi ya watu kwamba Simba hao wapo katika maeneo tofauti ya Iringa Mjini na kusababisha taharuki jambo ambalo si la kweli,” alisema.

Aliwapongeza Tanapa, wataalamu wa uwindaji na jamii ya wafugaji kwa doria za miguu, magari na helkopta wanazoendelea kuzifanya ili kuwanasa Simba waliobaki karibu na makazi ya watu na kuonekana katika eneo hilo la Kilolo.

Amewataka wananchi wanaoishi jirani na eneo hilo na jirani kutembea kwa makundi na kupunguza matembezi ya usiku wakati vikosi hivyo vikiendelea kuwasaka Simba hao.

Habari Zifananazo

2 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button