Simba yaacha pointi Mbeya

SIMBA wamezidi kuwa mbali na watani wao wa jadi Yanga baada ya kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya jana.

Mzamiru Yassin aliifungia Simba bao la uongozi dakika ya 15 na Tariq Seif kuisawazishia Mbeya City bao dakika ya 78.

Matokeo hayo yanaifanya Simba kusalia katika nafasi ya tatu kwa kufikisha pointi 28 nyuma ya Azam FC na Yanga zenye pointi sawa 29 huku Mbeya City ikiwa katika nafasi ya sita kwa pointi 19.

Simba pia iko mbele mechi mbili zaidi ya Yanga.

Awali, katika mchezo huo wenyeji Mbeya City walikuwa wakicheza kwa nidhamu kwa kuwaheshimu Simba wakilinda zaidi lango kitendo ambacho kiliwapa nafasi Simba kumiliki mpira na kushambulia zaidi lango lao.

Simba ilitengeneza nafasi zaidi ya mbili za kufunga kupitia kwa John Bocco, Mzamiru dakika za awali lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo ila baadaye dakika 15 Mzamiru akawafungia wekundu hao bao kufuatia pasi nzuri ya kisigino ya John Bocco.

Timu hizo zilikwenda mapumziko Simba ikiwa mbele kwa bao 1-0 ikiongoza pia, katika umiliki wa mpira.

Kipindi cha pili Simba ilifanya mabadiliko dakika ya 53 kwa kumtoa  Augustine Okrah na kuingia Kibu Denis.

Licha ya Simba kucheza vizuri kwa umiliki wa mpira bado walifanya makosa dakika ya 78 na kuwaruhusu Mbeya City kupata bao la kusawazisha lililofungwa na Seif baada ya pasi nzuri ya Awadh Salum.

Simba ilifanya mabadiliko mengine ikiwatoa Bocco na Mohamed Hussein dakika ya 85 na 89 na kuingia Habibu Kyombo na Pape Sakho ila hayakuzaa matunda kwani Mbeya City walionekana kurudi nyuma kulinda lango na kushambulia kwa kushtukiza hadi dakika 90 zilipokamilika wakitoka sare ya bao 1-1.

Mchezo mwingine ulichezwa kwenye Uwanja wa Liti mkoani Singida, ambapo Singida Big Stars iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMC.

Bao hilo pekee lilifungwa na Meddie Kagere katika dakika ya 39 baada ya kupokea krosi nzuri ya Nicolaus Gyan.

Singida imepanda kutoka nafasi ya saba hadi ya nne kwa kufikisha pointi 21 na KMC ikisalia katika nafasi ya 10 kwa pointi 14.

Habari Zifananazo

Back to top button