Simba, Yanga fainali ya kisasi CAF

Simba kusukwa upya

SIMBA na Yanga hazijamaliza kazi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika; na michezo yao ya leo dhidi ya Horoya ya Guinea na kesho Us Monastir ya Tunisia kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa ni kama fainali ya kisasi.

KWA NINI

Ni kama mchezo wa fainali kwa sababu Simba inahitaji pointi tatu ili kwenda hatua ya robo fainali.

Advertisement

Simba inashika nafasi ya pili katika Kundi C baada ya kucheza michezo minne na kati ya hiyo, imeshinda miwili dhidi ya Vipers ya Uganda na kufikisha pointi sita huku ikipoteza michezo miwili dhidi ya Horoya ugenini bao 1-0 na dhidi ya Raja Casablanca nyumbani wakifungwa mabao 3-0.

Kinara wa kundi ni Raja Casablanca ya Morocco iliyoshinda michezo yote 12, hivyo tayari imeshafuzu na inaonesha wazi haina mpinzani huenda akaendelea na ushindi katika michezo aliyobakiza kwani hana presha.

Simba imebakiza michezo miwili dhidi ya Horoya na Raja. Na muhimu zaidi ni huu wa leo dhidi ya Horoya  kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

 

Kikosi cha Yanga

Kama wekundu watashinda watafikisha pointi tisa ambazo zitampeleka moja kwa moja robo fainali na kwa hiyo Horoya yenye pointi nne hata ikishinda mchezo wake wa mwisho haitamfikia kwani itafikisha pointi saba.

Unaweza ukawa mchezo mgumu kwa kuwa Horoya yenye pointi nne nayo inahitaji ushindi ili kufufua matumaini yake ya kusonga mbele katika hatua hiyo.

Horoya inajua kabisa ikishinda dhidi ya Simba, mchezo wake wa mwisho itakutana na Vipers nyumbani kwake kwa hiyo itakuja kwa nguvu kutaka ushindi. Lakini pia, sio timu ya kubezwa, wana kikosi kizuri ndio maana wamefika hatua hiyo.

Ni muhimu Simba kushinda ili wakienda kumaliza mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Raja wasiwe na presha bali waende kumaliza kazi wakiwa na furaha na kucheza kwa burudani hata kama watapoteza.

Mchezo dhidi ya Horoya unawakumbusha Simba msimu wa mwaka 2018, waliwahi kuwa na mechi ya namna hiyo ya kuamua hatima yao ya kusonga mbele hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa.

Simba walifungwa mchezo wa kwanza ugenini dhidi ya Nkana FC ya Zambia mabao 2-1 walivyorudi Dar es Salaam walipindua meza kibabe na kushinda mabao 3-1.

Kwa kile ambacho waliwahi kufanya kipindi ambacho walihitaji matokeo ndicho kinatokea sasa, na wamejipanga kuhakikisha wanapindua meza.

 

KISASI

Ni mchezo wa kisasi kwa kuwa Simba ilipoteza mchezo wa kwanza bao 1-0 ugenini nchini Guinea hivyo leo wanahitaji kulipiza kisasi kwa kuhakikisha wanashinda ushindi wowote ilimradi uwape matokeo ya pointi tatu zitakazowasaidia kusonga mbele.

Kaulimbiu yao inasema ‘Tunaitaka robo fainali’ bila shaka wamedhamiria na wanataka kufanya mapinduzi. Wanasema kwa Mkapa hatoki mtu na hilo kwa wekundu inawezekana kama mashabiki wao watajitokeza na kujaza uwanja kuwatia moyo wachezaji, kama wachezaji watacheza kwa kujituma kama ilivyokuwa kwa michezo mingine iliyopita.

Simba wana kila sababu ya kushinda kwa sababu wana kikosi kizuri ambacho kimeonesha mapambano katika mechi zilizopita hivyo, wakiamua wanaweza.

YANGA

Yanga inatarajia kucheza na US Monastir ya Tunisia katika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kesho.

Monastir ni timu nzuri iliyoonesha ubora tangu mechi za awali na ndiyo iliyemtoa bingwa wa michuano ya Shirikisho, RS Berkane katika mechi za hatua ya pili ya mtoano kuelekea makundi. Walitoka sare ya kutokufungana ugenini kisha wakashinda kwao bao 1-0.

Ni timu inayocheza kwa akili hasa inapokuwa ugenini, hutafuta sare au ushindi na wamefanikiwa katika michezo minne waliyocheza, wameshinda mitatu na sare moja.

Haijapoteza mchezo wowote. Hawa ndio vinara wa Kundi D wakiwa wamefikisha pointi 10.

Yanga inakutana na Monastir wakiwa na njaa ya kufika robo fainali. Mchezo utakaoamua hatima yao. Mchezo unaofananishwa na fainali.

Ni mchezo wa kisasi pia, hasa baada ya mchezo wa kwanza ugenini Yanga kupoteza mabao 2-0. Mabao yote yakitokana na mipira iliyokufa, mipira ya adhabu. Wachezaji wengi wa Monastir ni warefu na waliwasumbua.

Yanga wanahitaji ushindi, wakishinda watafikisha pointi 10 ambazo kwa hakika wao na Monastir ndio watakaokwenda hatua ya robo fainali.

Kwa sababu TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) akishinda ugenini dhidi ya Real Bamako atafikisha pointi sita kisha mchezo wa mwisho dhidi ya Yanga akishinda kwao atafikisha pointi tisa ambazo hataweza kumfikia Yanga kama atashinda mechi na Monastir.

Lakini ikiwa Yanga atapata sare na Mazembe akashinda basi atakuwa kwenye presha kubwa kuelekea mchezo wa mwisho utakaowakutanisha, wenyeji watapata nguvu. Wote wawili wanaombeana mabaya kwenye matokeo yao.

Lolote linawezekana kwa Yanga kupata ushindi, inategemea watakuwa wamejiandaaje ndani na nje ya uwanja.

Jambo kubwa wanapaswa kujua ni kuwaheshimu wapinzani wao lakini pia, kuendelea kuonesha ubora kama ambavyo walifanya katika mechi zilizopita na kucheza kwa nidhamu kubwa.

Yanga ina muda mrefu haijafikia hatua ya robo fainali, hivyo kupata matokeo na kuvuka hatua hiyo itakuwa ni mafanikio mengine mapya na historia chini ya utawala mpya wa rais wao, Hersi Said anayetaka kufanya mapinduzi ya soka nchini.

Ushindi wa Yanga utachagizwa na mashabiki. Wana kaulimbiu yao inasema ‘Full shangwe, waje tumalizane’,  mashabiki wajitokeze kwa wingi kuujaza Uwanja wa Mkapa ili kila mmoja ashuhudie historia hiyo mpya kwao.

Ushindi wa Simba na Yanga kwa pamoja utakuwa ni faraja kwa mashabiki zao, wadau wa soka, Ligi Kuu Tanzania na serikali ambayo kwa namna moja ama nyingine inasapoti juhudi zao kuyafikia mafanikio.