Simba yanusa makundi Caf

TIMU ya Simba imetanguliza mguu mmoja hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Clube Desportivo Primeiro de Agosto ya Angola jana.

Mchezo huo wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa ulichezwa kwenye Uwanja wa Estádio 11 de Novembro jijini Luanda, Angola.

Simba waliandika bao lao la kwanza dakika ya 10 mfungaji akiwa Clatous Chama, aliyetumia vema pasi ya Augustine Okrah na kuwapa uongozi wageni hadi dakika 45 za kipindi cha kwanza zinatamatika, matokeo yalikuwa 1-0.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Simba kupata bao la pili dakika ya 63 lililofungwa na mlinzi wake wa kulia, Israel Patrick aliyetumia vyema pasi ya kiungo Sadio Kanoute, Wekundu wa Msimbazi waliendelea kutakata baada ya kuandika bao la tatu dakika ya 77 lililofungwa na Moses Phiri.

Clube Desportivo Primeiro de Agosto walipata bao lao la kufutia machozi dakika 78 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Dago Tshibamba, baada ya beki wa kati wa Simba, Kennedy Juma kuunawa mpira kwenye eneo la hatari.

Timu hizo zinatarajiwa kurudiana tena Oktoba 16, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa , Dar es Salaam, huku Simba ikihitaji sare ya aina yoyote ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mara ya mwisho Clube Desportivo Primeiro de Agosto, kucheza kwenye ardhi ya Tanzania ilikuwa mwaka 2021, ilipopoteza 7-5 mbele ya Namungo katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba msimu uliopita ilitolewa raundi ya kwanza na Galaxy ya Botswana baada ya kushinda mabao 2-0 ugenini kabla ya kufungwa 3-1 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa na kuangukia Kombe la Shirikisho, ambako iliishia robo fainali baada ya kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Habari Zifananazo

Back to top button