TIMU ya Simba imewasili Dar es Salaam asubuhi ya leo, ikirokea Luanda, Angola, ambako jana iliibuka na ushindi wa mabao 1-3 dhidi ya wenyeji Primeiro de Agosto katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Mchezo wa jana ambao ni wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa, mabao ya Simba yalifungwa na Clatous Chama, Israel Mwenda na Moses Phiri, wakati la wapinzani wao lilifungwa kwa mkwaju wa penalti na Dago Tshibamba.
Simba ambayo ilienda kwa ndege maalum ya kukodi iliwasili Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam, tayari kuanza maandalizi ya mchezo wa marudiano Oktoba 16, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa , Dar es Salaam.
Kocha Mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema bado kazi haijaisha na kwamba wanajipanga kwa ajili ya mchezo huo wa marudiano, ambao Simba itahitaji ushindi, au sare ya aina yoyote, au isifungwe zaidi ya mabao 2-0, ili kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.