Simba yataja sababu kuuzwa Chama

ALIYEKUWA Mtendaji Mkuu wa timu ya Simba, Crecentius Magori, amesema kuwa licha ya kuweka mkataba mnono wa miaka miwili ili kumzuia kiungo mshambuliaji wa timu hiyo Clatous Chama, nyota huyo aligoma na kuamua kutafuta changamoto mahala pengine.

Simba ilimsajili Chama mwaka 2018 kama mchezaji huru akitokea timu ya Lusaka Dynamos ya nchini Zambia mwaka 2018 ili kuimarisha kikosi chao kilichokuwa kikishiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tangu alipojiunga ameisaidia Simba kutwaa mataji nane, yakiwemo matatu ya Ligi Kuu, makombe mawili ya Kombe la Shirikisho la Azam pamoja na Ngao tatu za Jamii, huku akiifikisha robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili.
Akizungumza jana Magori, alisema kuondoka kwa Miquisonne haikuwa ajabu sababu ofa ilikuwapo mezani muda mrefu, lakini Chama hawakuwa tayari kumuacha aondoke ndio maana walikuwa wameshampa mkataba mpya wa miaka miwili, ambao ulikuwa wa pesa nyingi, ambazo hapa nyumbani hakuna timu ingweza kumpa.
“Mkataba ambao tulikuwa tumemuandalia Chama, angekuwa ghali na hakuna mchezaji ambaye angekuwa analipwa kiasi kile hapa nchini, lakini akashinikiza kuondoka ndipo tukamuacha aondoke,” alisema Magori.
Alisema kuwa hata muwekezaji mkuu Mohamed Dewji alikataa Chama kuondoka, lakini kiungo huyo alisisitiza kwamba anataka kuchukua ofa mpya ili akatafute changamoto mahala pengine.