SIMBA imetakata nyumbani baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jana.
Ushindi huo unaifanya Simba kufikisha pointi 63 na kuendelea kusalia nafasi ya pili nyuma ya Yanga wanaoongoza wakiwa na pointi 68, huku matokeo hayo yakivuruga ubingwa wa Yanga, ambao kama ingeshinda ingezidi kuukaribia.
Simba walipata bao la kwanza katika dakika ya pili mfungaji akiwa ni Henock Inonga akifunga kwa kichwa akimalizia mpira wa krosi uliopigwa na Shomari Kapombe.
Dakika ya 31 Simba waliandika bao la pili lililofungwa na mshambuliaji Kibu Denis kwa shuti kali baada kupokonya mpira mlinzi wa Yanga,Bakari Mwamnyeto na kuachia shuti kali lililomshinda kipa Djigui Diara.
Simba walikaribia kupata bao jingine dakika ya 29 baada ya Jean Baleke kupiga mpira uliogonga nguzo na kurejea ndani na kuokolewa na beki Bakari Mwamnyeto.
Mwamuzi Jonesia Rukyaa dakika ya 29 alimuonyesha kadi ya njano mshambuliaji Kibu Denis kwa kumfanyia madhambi Khalid Aucho.
Mshambuliaji Fiston Mayele alikaribia kuipatia bao Yanga dakika ya 35 baada ya kupiga shuti kali lakini likaokolewa na kipa wa Simba, Ali Salim.
Simba walifanya shambulizi la kushtukiza dakika ya 44 mshambuliaji wake Jean Baleke akiwa ana kwa ana na kipa Djigui Diara lakini kukosa umakini kukamfanya akose bao hilo.
Hadi mwamuzi Jonesia Rukyaa anapuliza kipyenga kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Dakika 46 kocha wa Yanga Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko kwa kuwatoa Jesus Moloko, Yannick Bangala na Salum Abubakar huku nafasi zao zikachukuliwa na Mudathir Yahya, Stefan Aziz Ki na Tuisila Kisinda.
Mabadiliko hayo yaliongeza chachu kwenye kikosi cha Yanga ambacho kilianza kuliandama lango la Simba; Aziz Ki alikaribia kuipatia timu yake goli katika dakika ya 60 kwa mpira wa adhabu lakini shuti lake likagonga ukuta wa safu ya ulinzi ya Simba.
Dakika ya 66 Aziz alishindwa kuipatia bao timu yake baada kukutana ana kwa ana na kipa Ali Salim lakini mpira wake ukapaa juu ya lango.
Mwamuzi Jonesia Rukyaa, dakika ya 68 alimuonyesha kadi ya njano kipa Ali Salim kwa kupoteza muda.
Kocha wa Yanga Nasreddine Nabi alifanya mabadiliko mengine dakika ya 70 kwa kumtoa Kennedy Musonda na nafasi yake ikachukuliwa na Benard Morrison ili kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.
Kocha wa Simba Roberto Oliveira, alifanya mabadiliko ya kwanza dakika ya 74 kwa kumtoa Erasto Nyoni na nafasi yake ikachukuliwa na Nassoro Kapama ili kuimarisha eneo la kiungo.
Simba walifanya mabadiliko mengine dakika ya 82 kwa kumtoa Jean Baleke nafasi yake ikachukuliwa na John Bocco, huku pia akimtoa Kibu Denis dakika ya 94 na kumuingiza Moses Phiri.
Hadi mwamuzi Jonesia Rukyaa anapuliza kipyenga kumaliza dakika 90 Simba walikuwa mbele kwa mabao 2-0.
Mara ya mwisho Simba kupata ushindi kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara ilikuwa mwaka 2019 waliposhinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Meddie Kagere.