Simba yawaomba radhi mashabiki

MWENYEKITI wa Bodi ya Wakurugenzi wa Klabu ya Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amewaomba radhi wanachama na mashabiki wa klabu hiyo kwa kushindwa kutwaa taji lolote ikiwa ni msimu wa pili mfululizo.

Try Again aliyasema hayo jana akieleza kuwa kwenye mpira hali hiyo ni ya kawaida na haipaswi kunyoosheana vidole katika kipindi hiki na badala yake wanapaswa kujipanga kwa ajili ya msimu ujao.

Simba ambayo jana ilikuwa ikiumana na Ruvu Shooting inakaribia kuupoteza ubingwa wa Ligi Kuu Bara endapo Yanga leo itashinda mechi yake dhidi ya Dodoma Jiji ambapo watafikisha pointi 74 ambazo hazitafikiwa na timu yoyote.

Advertisement

Pia, Wekundu hao wiki mbili zilizopita walitolewa katika hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa matuta 4-3 na Wydad Casablanca ya Morocco kabla ya kufungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye nusu fainali ya Kombe la FA (ASFC) siku tano zilizopita.

Akifafanua kilichowaangusha kukosa makombe hayo, Try Again alisema ni majeraha yaliyokuwa yakiwaandama wachezaji wao, wachezaji wapya waliowasajili walioshindwa kuonesha ubora na ugumu wa mechi za Ligi Kuu.

“Kwa niaba ya Bodi ya Wakurugenzi, nachukua nafasi hii kuwaomba radhi Wanasimba wote, hatukuwa na msimu mzuri sababu tumekosa mataji yote. Tumekuwa na changamoto ya majeruhi kikosini, wale tuliowaongeza pia wameshindwa kuonesha ubora lakini ndio mpira tunajipanga kwa msimu mpya,” alisema Try Again.

Simba ambayo imetwaa ubingwa wa ligi mara nne mfululizo kabla ya kuchukuliwa na Yanga msimu uliopita, pia mwanzoni mwa msimu huu ilipoteza Ngao ya Jamii kwa kufungwa mabao 2-1 na Yanga kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.

1 comments

Comments are closed.