Simba yazinduka

SIMBA imezinduka kutoka katika usingizi mzito baada ya jana kuibuka na ushindi wa mabao 3-1, dhidi ya Polisi Tanzania katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Ushirika, Moshi.

Kabla ya mchezo huo, Simba ililazimishwa sare ya bao 1-1 na Mbeya City Uwanja wa Sokoine Mbeya matokeo ambayo yaliwasononesha mashabiki wa timu hiyo na kuongeza tofauti ya pointi kati yao na vinara wa ligi hiyo, Yanga.

Ushindi huo wa jana umeipandisha Simba hadi katika nafasi ya pili wakifikisha pointi 31, na kuishusha Azam FC ambayo kabla ya mchezo wa Simba ilikuwa nafasi ya pili, lakini Azam inaweza kurudi kwenye nafasi ya pili endapo itashinda mchezo wake dhidi ya Coastal Union uliotarajiwa kucheza jana kuanzia saa 1:00 usiku Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salaam.

Mabao ya Simba katika mchezo huo yalifungwa na nahodha John Bocco dakika ya 33 na Moses Phiri aliyefunga mabao mawili katika dakika za 43 na 53, huku bao la kufutia machozi la Polisi Tanzania likifungwa na Zuber Khamis dakika ya 90.

Kwa Phiri mabao hayo mawili aliyofunga jana yanamfanya afikishe idadi ya mabao nane kwenye ligi na kukaa nafasi ya pili katika orodha ya wanaoongoza kwa ufungaji nyuma ya Fiston Mayele wa Yanga mwenye mabao 10.

Katika mchezo huo wenyeji Polisi Tanzania ndio waliuanza mchezo kwa kasi na kuliandama lango la Simba ambapo walifanikiwa kupata nafasi mbili za wazi lakini washambuliaji wake Vitalis Mayanga na Idd Kipwagile wakashindwa kuzitumia.

Baada ya kuhimili mashambulizi hayo Simba walicharuka na kuanza kupanga vyema mashambulizi yao ambapo dakika ya 33 Bocco alifunga bao la kwanza kwa pasi ya Shomari Kapombe na dakika mbili kabla ya kwenda mapumziko Phiri akafunga bao la pili akiunganisha pasi ya Cletus Chama.

Kipindi cha pili kilianza kwa Simba kuendeleza mashambulizi katika lango ya Polisi na dakika ya 53 Phiri alifunga bao la tatu na kuwakatisha tamaa mashabiki wa Polisi waliokuwa na matumaini ya kusawazisha ingawa wachezaji waliendelea kupambana na kufanikiwa kupata bao la kufutia machozi kupitia kwa Zuber dakika ya 90.

Bao hilo lilionekana kuwapa nguvu Polisi lakini Simba nao walikuwa imara na wenyeji wakajikuta wanapoteza mchezo huo ambao ni wa kwanza msimu huu kucheza kwenye uwanja wa Ushirika baada ya kufungiwa kwa muda mrefu kutokana na kutokidhi vigezo.

Habari Zifananazo

Back to top button