Simbachawene anyoosha kiburi cha mwanaye

WAZIRI wa Nchi, Ofi si ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), George Simbachawene ameliagiza Jeshi la Polisi kumchukulia hatua za kisheria bila huruma mtoto wake kutokana na kosa la usalama barabarani alilolifanya.

Simbachawene alilazimika kutoa kauli hiyo, baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii zikimwonesha akitoa lugha ya kuudhi kwa watu aliogonga magari yao pamoja na askari wa usalama barabarani. Katika video hizo, alisikika mmoja wa watu ambao gari lake mtoto huyo wa Simbachawene (jina halijafahamika), aliligonga akilalamika kuwa baada ya kumgonga alisema yeye ni mtoto wa Waziri Simbachawene hakuna mtu wa kumfanya chochote.

Kwa mujibu wa raia huyo, alisema kijana huyo aligonga magari mawili na kukimbia na hata walipomkamata na kumhoji alitoa maneno ya lugha ya kuudhi. Katika taarifa yake, Simbachawene alikiri kuwa kijana huyo ni mtoto wake na kuliagiza jeshi hilo la polisi achukuliwe hatua kwa makosa aliyoyafanya.

“Nimeiona clip inayozunguka kwenye mitandao ya kijamii, nakiri kuwa huyo ni kijana wangu ambae ni mtu mzima anajitegemea na ana familia yake…. Nimemwagiza Mkuu wa kituo kwa sababu amekosa adabu kwa Jeshi la Polisi na ametenda kosa la usalama barabarani, ashughulikiwe bila huruma kwa mujibu wa sheria …,” alisema.

Aidha, aliomba radhi kwa walioathirika na mkasa huo lakini pia kwa Jeshi la Polisi na Watanzania wote. “Binafsi naomba radhi sana kwa walioathirika na mkasa huo lakini pia kwa Jeshi la Polisi na Watanzania wote. Poleni kwa usumbufu wowote mlioupata. Ni Mimi. George B. Simbachawene (MB),” aliandika.

Habari Zifananazo

Back to top button