MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema mkoa huo unajiandaa kuanza kutengeneza simu janja.
Kunenge amesema hayo mjini Kibaha kwenye kikao maalumu cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji Kibaha.
Kikao hicho kilijadili hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2021-2022.
Alisema ujenzi wa kiwanda hicho ni matunda ya uwekezaji na kwamba maandalizi ya utengenezaji wa simu hizo yanaendelea vizuri na muda si mrefu simu hizo zitaanza kutengenezwa.
“Pwani tumefika mbali kwenye suala la uwekezaji ambapo tutakuwa wa kwanza kuzalisha simu za smart phone (simu janja) na tumepongezwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Mkoa wa Pwani wako vizuri kwenye suala la uwekezaji,” alisema Kunenge.
Mwaka 2021, Rais Samia Suluhu Hassan alizindua kiwanda cha kutengeneza nyaya za mkongo wa mawasiliano cha Raddy Fibre Manufacturing (T) Ltd Mkuranga mkoani humo na sasa kipo kwenye maandalizi ya kuzalisha simu hizo.
Kwa mujibu wa Kunenge, mkoa una viwanda 1,522 vikiwamo vikubwa 27. Alisema halmashauri zinapaswa kuweka maandalizi mazuri ya uwekezaji na kuanzisha vyanzo vipya vya uwekezaji.
“Kikubwa mnachopaswa kukifanya ni kupambana na migogoro ya ardhi ambayo kwa mkoa ni mingi na haipaswi kuwepo kwani mwekezaji asingependa kuona migogoro,” alisema Kunenge.
Comments are closed.