TANZANIA imeendelea kushuhudia mabadiliko makubwa ya sekta ya mawasiliano kutokana na ongezeko la laini za simu, watumiaji wa huduma za intaneti, huduma za kutuma na kutoa fedha kwa njia ya simu.
Kutokana na maendeleo hayo, zipo faida na changamoto ambazo watumiaji wa huduma za mawasiliano wamekuwa wakizipitia hususani kupanda kwa gharama za bando la intaneti na kuisha haraka.
Moja ya sababu ya kuisha haraka kwa data inatajwa kuwa uwezo wa kifaa cha mawasiliano ikiwemo simu janja, kompyuta mpakato ambazo zimetengenezwa kwa ufanisi wa hali ya juu na kwamba matumizi ya mtu yatachangia kuisha haraka kwa vifurushi anavyojiunga navyo.
Mkurugenzi wa Masuala ya Kisekta wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Dk Emmanuel Manasseh, anasema gharama za data kwa taarifa za Aprili mwaka huu ni kuanzia Sh 1.5 kwa Megabaiti moja (Mb) hadi Sh 9.35 kwa Mb.
Dk Manasseh anasema kuwa vifaa vya mawasiliano vinatengenezwa na kampuni chache duniani na kwamba bei ya vifaa hivyo, haiangalii uchumi wa nchi husika.
Anasema kuwa ili Watanzania wote wapate huduma hizo za data, uwekezaji mkubwa unahitajika ili nchi nzima ipate mawasiliano bila kujali uchumi na idadi ya watu.
“Stady (utafiti) za TCRA zinaonesha kuwa gharama halisi za kuuza data ni kati ya Sh 2.03 Mb ambazo mtoa huduma anaweza kuuza na kurudisha gharama za uendeshaji na Sh 9.35 Mb ni ambazo mtoa huduma anaweza kuendeleza uwekezaji,” anasema Dk Manasseh.
Pia anasema sababu za kuisha kwa haraka kwa data ni kubadilika kwa teknolojia ikiwemo kasi na muda unaotumika kupakua na kupakia data, ubora wa vifaa vya teknolojia na kuongezeka kwa ukubwa wa picha.
Anaeleza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia vifurushi vyote vinavyoenda sokoni na kwamba mteja hununua kulingana na mahitaji yake na kwamba bei ya huduma za data kwa nchi za Afrika Mashariki, wastani wa gharama ni Dola za Marekani 0.75 kwa Gigabaiti (GB) moja sawa na Sh 1,725 hivyo Tanzania ni miongoni mwa nchi sita kati ya 52 zenye gharama nafuu za data.
Hata hivyo, kutokana na malalamiko ya mara kwa mara ya watumiaji wa huduma za mawasiliano hususani wa simu za mikononi, serikali imeamua kuja na tathmini itakayoweka bei elekezi za vifurushi vya simu (bundle).
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anasema serikali kupitia TCRA iko katika hatua za mwisho kukamilisha tathmini ya gharama za huduma za mawasiliano nchini na kwamba wanategemea kushusha gharama za vifurushi hivyo.
Nape anasema kwa muda mrefu kumekuwa na mjadala wa vifurushi mbalimbali vya simu ikiwemo intaneti huku watumiaji wakihoji hatua zinazochukuliwa na serikali, hivyo amewataka watoa huduma za mawasiliano kutobadilisha vifurushi vya simu hadi pale watakapotoa bei elekezi Januari 2023.
Anasema katika tathmini hiyo inaangalia uwekezaji uliofanywa na kampuni za simu na kodi wanayolipa ili kuwa na bei elekezi na mategemeo yao ni kushusha gharama hizo kwa kiasi fulani.
“TCRA imekuwa ikifanya tathmini kila baada ya miaka mitano na tathmini ya mwisho imefanyika mwaka 2018 na tathmini ilielekeza gharama za huduma hizo ziwe kati ya Sh 2.03 na 9.35. Lakini watumiaji wengi wa huduma hizi wameeleza kuwa hawafurahishwi na huduma za mawasiliano zinazotolewa na hakuna mawasiliano mazuri kati ya watumiaji na watoa huduma,” anasema Nape.
Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, Dk Jabiri Bakari anasema wastani wa gharama za vifurushi vya simu zilikuwa Sh 7.8 kwa kupiga simu za ndani ya mtandao Septamba, 2022 kutoka Sh 7.7 Juni mwaka huu.
“Pamoja na ongezeko hili dogo gharama bado ni chini ukilinganisha na vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine, wastani wa vifurushi vya simu kwenda mitandao mingine ilikuwa Sh 8.1 Septemba 2022 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh 7.6 Juni mwaka huu,” anasisitiza.
Pia anasema kuwa kwa mtu ambaye anatumia simu yenye uwezo mkubwa ni lazima atatumia data nyingi pindi anapopakua au kupandisha taarifa kwenye ukurasa wake.
Anasema kuwa watu wanaopakua video kwenye simu wanapewa fursa ya kuchagua kiwango cha data anachokitaka na ubora wa video hivyo anapokubali kuchukua video yenye ubora wa juu kabisa ambao ni zaidi ya Megabaiti 150 hata data zake alizonunua zitakwisha haraka.
“Kwa kifupi ni kuwa matumizi yako ndio yatafanya bando lako likae kwa muda mfupi au mrefu sambamba na kifaa chako cha mawasiliano. Kwa mfano kuna simu za kawaida ambazo hazipokei taarifa iliyozidi Megabaiti nane hivyo na nyingine zinapokea zaidi ya Mb hizo, hivyo uchaguzi wa viwango vya data kwa taarifa unayoitaka ni muhimu,” anasisitiza Dk Bakari.
Anaeleza kuwa wanaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia wawekezaji na watumiaji wa huduma za mawasiliano na kwamba watatoa rasilimali za masafa ili kuhakikisha huduma bora za mawasiliano na kushusha gharama za mawasiliano.
Katika ripoti ya utendaji wa sekta ya mawasiliano kwa kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2022/23 inaonesha kuwa kuna ongezeko la asilimia 3.4 ya laini za simu huku matumizi ya huduma za intaneti, mitandao ya kijamii na huduma za kifedha kwa mtandao zikiongezeka kutoka miamala ya Sh bilioni 349.9 hadi Sh bilioni 366.1 Septemba mwaka huu.
Pia inaonesha kuwa idadi ya laini za simu zinazotumika hadi kufikia Septemba mwaka huu ni milioni 58.1 kutoka milioni 56.2 Juni mwaka huu. Katika takwimu zilizotolewa zinaonesha kuwa mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Tabora inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya laini zinazotumiwa na watu na zinazotumika kwa ajili ya mawasiliano kwa mashine.
Mpaka sasa Watanzania wanaotumia simu janja ni asilimia 27 pekee. Dk Bakari anasema: “Dar es Salaam ina laini milioni 9.7, Mwanza (milioni 3.7), Arusha (milioni 3.4), Mbeya (milioni 3.08) na Tabora (milioni 3.06), mwelekeo wa usajili kwa miaka mitano iliyopita unaonesha ongezeko la asilimia nane kwa mwaka. Kuenea kwa laini miongoni mwa watu kumeongezeka kwa asilimia nne kwa mwaka kwani mwaka 2017 ilikuwa asilimia 78 na mwaka 2021 ni asilimia 91.”
Anasema Tanzania inazidi kuendeleza mfumo jumuishi wa kifedha kutokana na kuongezeka kwa watumiaji wanaofanya miamala kupitia simu za mkononi na kwamba takwimu zinaonesha Septemba mwaka huu huduma za fedha zimeongezeka kutoka Sh milioni 38.0 Juni hadi Sh milioni 39.5 Septemba mwaka huu.
“Vodacom inaongoza kwa kuwa na miamala ya asilimia 39, ikifuatiwa na Tigo yenye asilimia 25, Airtel asilimia 23, Halotel asilimia tisa na TTCL asilimia nne.
Akaunti za fedha zimeongezeka kwa asilimia 1.5 kwa miezi tisa iliyopita kuanzia Januari hadi Septemba wakati miamala ikiongezeka kwa asilimia mbili kutoka Sh bilioni 10.3 hadi Sh bilioni 12.7,” anafafanua.