SIMULIZI YA KUSIKITISHA YA ASIA
Mimba umri mdogo, kuondolewa kizazi, ulemavu miguu vyasitisha ndoto zake

UMASKINI umechangia kuzima ndoto za Asia Patric (21) ambaye alijikuta akikatwa miguu na vidole baada ya kukosa shilingi 150,000 kwa ajili ya matibabu ya kusafishwa kizazi baada ya mimba kuharibika.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto (UNICEF) na Benki ya Dunia iliyotolewa Oktoba 2020 imekadiria kuwa mtoto 1 kati ya 6 sawa na watoto milioni 356 duniani kote, walikuwa wanaishi katika umaskini uliokithiri kabla ya janga la Covid-19.
Utafiti uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) 2017-18 unaonesha kuwa wastani wa matumizi ya kaya moja kwa mwezi kwa Tanzania Bara ni shilingi 416,927. Kwa maeneo ya mijini ni Sh 534,619 na vijijini ni Sh 361,956.
Asia, ni miongoni mwa mabinti ambao wamejikuta kwenye majanga kutokana na hali ya umaskini katika familia yake na kujikuta akipoteza viungo vyake na kubaki mlemavu.
Akizungumza na HabariLEO, Asia anasema amekuwa mlemavu mwenye kidole kimoja tu, baada ya vyote tisa mkononi kukatwa sambamba na miguu yake yote miwili.

Akisimulia Asia anasema, akiwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne hakufanikiwa kuendelea na shule kutokana na changamoto za kifamilia na hivyo kujikuta akiangukia mikononi mwa Rashid Musa tangu mwaka 2018 ambaye waliishi kama mume na mke licha ya kwamba hawakubahatika kufunga ndoa.
Anasema mwaka huo, akiwa na miaka 18, alifanikiwa kupata ujauzito, ambao aliutunza akiwa na matarajio ya kujifungua salama na kupakata mtoto wake wa kwanza.
Isivyokuwa bahati mwanzoni mwa Aprili mwaka huo, akiwa na ujauzito wa miezi mitano, akiwa eneo la nyumbani kwao Buzuruga, alikanyaga kijiwe na kuteleza na kuangukia tumbo.
“Kwetu Mwanza tumezungukwa na mawe, hiyo siku sitakaa niisahau ilikuwa ni asubuhi nikiwa nimetoka kuamka, ile natoka nje kuna kajiwe nikakanyaga nikajikuta nimeteleza na kuanguka.
“Kumbe kile kitendo cha kuanguka mimba yangu iliharibika kwani baada ya muda kidogo nilianza kupata maumivu kwenye tumbo na damu zikaanza kunitoka, nilienda hospitali baada ya kuangaliwa na daktari niliyemkuta alinijulisha mimba yangu imetoka na hivyo natakiwa kutoa shilingi 150,000 ili aweze kunisafisha.
Anaongeza kusema: “Kwa wakati ule kutokana na hali ya familia yetu hatukuweza kumudu gharama hizo na ndipo ikatulazimu kurudi nyumbani nikiwa katika hali ya maumivu makali.
Anasema baada ya siku mbili, mmoja wa majirani zake alijitolea kumpa fedha na ushauri wa dawa ya kutumia itakayosaidia kumsafisha.
“Kati ya majirani niliokuwa nao akatokea mama mmoja akaniambia Asia kwa nini unateseka, akanipa shilingi 30,000 akaniambia tuma mtu akakununulie vidonge, mimi sikujua ni vidonge gani kwa sababu aliandika yeye na akamtuma mtoto akavinunue dukani, lakini baada ya kunywa dawa hizo sikupata unafuu wowote na hali ikazidi kuwa mbaya.
Anasema aliendelea kugugumia maumivu kwa siku kadhaa huku hali ikizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa katika Hospitali ya Sekou Toure.
Hata hivyo, baada ya kufikishwa Sekou Toure kutokana na hali yake ilivyokuwa walimpa rufaa ya kwenda Hospitali ya Rufaa ya Bugando.
Anasema baada ya kufikishwa Bugando, madaktari walimfanyia uchunguzi na kushauri kuwa anatakiwa kufanyiwa upasuaji wa kukiondoa kizazi, kwani kimeoza kabisa na kikiachwa anaweza kupoteza maisha.
Anakumbuka ilikuwa Aprili 17, 2018 alipofanyiwa upasuaji wa kuondoa kizazi chake na baada ya hapo akahamishiwa chumba cha wagonjwa wa uangalizi maalumu (ICU) kwa ajili ya uangalizi.
“Nikiwa ICU nilianza kuona vidole vyangu vya miguu na mikono vinavimba, vinasambaa na kuanza kuwa vyeusi, baadaye ule uvimbe ukapasuka na kutoa maji. baada ya maji, vikatoa usaha na harufu,” anasimulia Asia.
Anasema miguu yote miwili kuanzia vidoleni hadi karibu na goti ilivimba na kutoa maji, ngozi ikaanza kudondoka na usaha ukachuruzika.
“Nilikuwa na maumivu makali na si hivyo tu, nilihitaji sindano kwa kila baada ya saa moja, ambayo iligharimu Sh 500,000 kwa ajili ya kuzibua mishipa iliyoziba. Lakini familia yangu ni duni, hatukuweza kumudu hizo gharama,” anasema.
Baadaye miguu na mikono iliendelea kuoza na kubaki mifupa mitupu, kwani ngozi iliisha hadi ukiugonga mfupa kwa kisu huyasikii maumivu.
“Nakumbuka Mei 21, 2018, nilifanyiwa upasuaji wa kukata miguu yangu yote na vidole tisa,” anasema huku akilia. “Niliumia sana na sikuwahi kufikiria nitakuwa katika hali hii.”
Lakini anasema licha ya kukatwa miguu hiyo, baada ya muda mguu wa kushoto uliendelea kuoza na ikabidi arudishwe tena hospitali na mguu huo ukakatwa tena juu zaidi.
Anasema baada ya upasuaji huo wa pili wa viungo, alianza kupona lakini hakuruhusiwa kutoka hospitali kwa sababu hakuwa na fedha za kulipa gharama za matibabu.
“Nilikaa hospitali tangu Aprili, 2018 hadi Agosti 17, 2018 ndipo nilipotoka baada ya mama kupata msaada wa fedha za kulipa deni la hospitali kutoka kwa wasamaria,” anasema.
ASIA NA MAISHA MAPYA BILA VIUNGO
Baada ya Asia kuruhusiwa kurudi nyumbani, alianza maisha mapya bila viungo akitegemea msaada wa mama yake, kula, kuoga, kujisaidia, kuvaa na kila shughuli muhimu ya mwili wake, kwani hakuwa na miguu yote na mikononi akibakiwa na kidole gumba kimoja tu.
“Nilikuwa ni mtu wa ndani tu, kwa sababu nyumbani kwetu ni Buzuruga milimani na nyumba yetu ipo kwa juu sana, nilikuwa mtu wa kukaa, kuoga, kula ndani, ukitaka kuota jua nje inabidi kubebwa na kuwekwa mlangoni ndio ulione jua,” anasema.
DAKTARI ANENA
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Idara ya Magonjwa ya Uzazi na Kinamama, Said Ali, akizungumzia suala hilo la Asia anasema: “Sina hakika na dawa aliyopewa, ila ninachokiona Asia alipata ‘cellulitis’ ambapo seli za mwili zilikufa baada ya mishipa ya damu kuziba.
Akifafanua zaidi anasema kuchelewa kupata matibabu, huenda Asia alipata maambukizi katika mfuko wa kizazi, hali iliyosababisha kizazi kuharibika hadi kuondolewa.
“Maambukizi katika mfuko wa kizazi, yaani ‘sepsis’ naweza kusema ndio chanzo. Maambukizi haya husambaa kwa haraka na ndio sababu kupata ‘cellulitis’, pale mishipa ya damu inaziba, seli za mwili zinakufa.
“Madaktari waliomhudumia walifikia hatua ya kuamua kumkata viungo vya miguu na mikono kwa kuwa itakuwa walibaini tayari maambukizi yametoka kwenye kizazi, yakasambaa miguuni na tayari yalipanda kwenye vidole ili kumwokoa maisha yake ikalazimu kumkata,” anasema Dk Said.
Anasema, daktari wa awali mara ujauzito ulipotoka alipaswa kumpa huduma ili aokoe maisha yake kwanza kisha suala la fedha lingefuata baadaye.
APATA MSAADA
Anasema mama yake Asia, alikutanishwa na Flora Lauwo maarufu ‘Flora Nitetee’ ambaye anasaidia watu wenye matatizo mbalimbali na kuanzia hapo alipata msaada wa viungo bandia.
“Kupitia mitandao ya kijamii ya mamii (akimaanisha Flora Lauwo), nilisaidiwa na wasamaria wema ambao walinichangia fedha na nikanunuliwa miguu bandia Februari 2019,” anaongeza.
Anasema baada ya kupona, Flora alimchukua na kuanza kumpa mafunzo ya kufanya ‘makeup’ katika saluni yake.
“Nakumbuka siku hiyo nilikwenda kazini kwake, akaniambia, Asia hebu jaribu kushika hii brashi, alipoona naweza angalau kushika brashi bila vidole, akaniambia niende kesho kuanza mafunzo,” anasema huku akionesha tabasamu usoni lililochanganyika na huzuni.
CHANGAMOTO YA AJIRA
Asia anasema licha ya kufanikiwa kufuzu mafunzo ya upambaji, lakini bado amekuwa akipata changamoto ya ajira kwa vile wengi wanavyomwona katika hali ile ya ulemavu wanasita kumwajiri.
“Ni kweli watu wanauona uwezo wangu, lakini wanasita kuniajiri kwa sababu wanapata wasiwasi iwapo nitataka kujisaidia, nikiumwa ghafla na pia ili nimpambe mtu, natakiwa kukaa kwenye kiti kwa sababu siwezi kusimama kwa muda mrefu,” anasema na kuongeza: “Maumivu ya miguu bado yananisumbua, hasa ninapotembea muda mrefu au kusimama, pia mara kadhaa miguu hunichubua na kusababisha vidonda,” anasema.
Hata hivyo, licha ya changamoto hiyo, Asia anasema: “Nina uwezo, nimejikubali, nitafanya chochote, licha ya maumivu makali niliyonayo.”
Anita Samson wa Shirika la Wadada Solution la jijini Mwanza, kwa kushirikiana na Pathfinder International wanafanya kazi na vijana na kuwasaidia kuwapa elimu ya afya ya uzazi kwa kuepuka mimba za utotoni ambazo zinahatarisha maisha yao.
“Tumefanya kazi na Asia na kumpa stadi za maisha ikiwamo elimu ya ujasiriamali ili aweze kusonga mbele,” anasema Anita.