Singida, Mtibwa Sugar zataka Ligi Kuu

TIMU ya soka ya Singida Big Stars, imeendeleza wimbi la ushindi nyumbani kwenye Uwanja wa Liti baada ya jana kuibukana ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Mbeya City.

Ushindi huo unaifanya Singida kuwa kwenye tatu bora katika msimamo ikiwa na pointi sita sawa na Yanga na Simba inayoongoza msimamo huo zikitofautiana uwiano wa mabao.

Katika mechi ya kwanza, Mbeya City ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya 50 mfungaji akiwa Sixtus Sabilo, Singida ilisawazisha bao hilo dakika ya 53 kupitia kwa Dario Federico. Federico alifunga bao hilo kwa mkwaju wa penalti iliyotolewa na mwamuzi Ahmada Simba wa Kagera kwa madai ya mchezaji wa Singida kufanyiwa madhambi eneo la hatari.

Bruno Gomes aliifungia Singida bao la ushindi katika dakika ya 61. Nayo Mtibwa Sugar imeutumia vema Uwanja wa Manungu Complex baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Ruvu Shooting kutoka mkoani Pwani.

Mabao ya Mtibwa Sugar kwenye mchezo huo yalifungwa na Nassor Kiziwa katika dakika ya 23 na 57 wakati bao la kufutia machozi la Ruvu Shooting lilifungwa na Abalkassim Suleiman dakika ya 47. Katika mechi nyingine, Polisi Tanzania imeshindwa kutamba Uwanja wa nyumbani wa Sheikh Kaluta Amri Abeid, jijini Arusha baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na KMC.

Polisi Tanzania walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya pili na Ally Kipemba kabla ya Matheo Anthony kusawazisha dakika ya tano, Chilo Mkama aliwapa uongozi wenyeji dakika ya 10 lakini Matheo aliisawazishia timu yake dakika ya 47 na kufanya mechi kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Habari Zifananazo

Back to top button