MIKOA ya Singida, Tabora na Shinyanga imebainisha fursa mbalimbali za uwekezaji katika sekta za viwanda, kilimo, mifugo, asali, madini, afya, elimu na kutaka wawekezaji wa ndani na nje kuchangamkia fursa hizo.
Hayo yalibainishwa na viongozi wa mikoa hiyo wakati wa mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom jana.
Miongoni mwa viongozi walioshiriki mkutano huo ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk Batilda Buriani aliyesema kuwa asilimia 46 ya Mkoa wa Tabora ni misitu ya asili na hifadhi, hivyo kuna fursa ya kujenga viwanda vinavyohusiana na mazao ya nyuki.
Dk Buriani alitaja fursa hizo za uwekezaji kwenye sekta ya viwanda mkoani humo kuwa ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kutengeneza mizinga ya kufugia nyuki, viwanda vya kuzalisha mazao ya nta na asali pamoja na viwanda vya kutengeneza vifungashio vya chupa kwa ajili ya kuhifadhia asali.
Wasaidizi wake akiwamo Katibu Tawala wa mkoa huo, Dk John Mboya, walizitaja fursa nyingine za uwekezaji kuwa ni pamoja na uwekezaji katika ujenzi wa shule na vyuo mbalimbali vikiwamo vyuo vikuu, ujenzi wa hospitali, hoteli za kitalii na kumbi za mikutano.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, Katibu Tawala Msaidizi wa mkoa huo, Stanslaus Choaji, alisema vipo viwanda 221 vya kusindika alizeti ambavyo vinahitaji tani 632,000 kwa mwaka lakini uzalishaji wa mkoa haufikii mahitaji hayo.
Choaji alitoa wito kwa wawekezaji wa ndani na nje kwenda kuwekeza kwenye uzalishaji wa zao la alizeti kwa kuwa kuna ardhi nzuri na ya kutosha na fursa ni kubwa.
Fursa nyingine za uwekezaji mkoani Singida ni uzalishaji wa zao la korosho kwa kuwa tayari kuna ekari 3,000 walizosafisha na zinahitaji wawekezaji.
Kwa upande wa Mkoa wa Shinyanga, fursa za uwekezaji zilizopo ni pamoja na ujenzi wa viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo hususani mpunga, mahindi, mihogo, njugu mawe, alizeti, pamba, mkonge na mengineyo.
Akizingumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Sophia Mjema, Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu, Chila Moses, alisema Shinyanga kuna ardhi nzuri inayofaa kuzalisha mazao hayo na mazao mengine mengi, hivyo akatoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa hiyo.