Sitaki mwenziwe basi!

MOJA katika habari ya kimichezo ambayo imetikisa mwaka huu na inaweza kuwa ya kufungia mwaka ni kwa mchezaji Feisal Salum Abdallah kuamua kutafuta maisha bora zaidi ya maslahi ya soka.

Wakati Feisal akiamua kutafuta ahueni ya maisha kwa kwenda kutafuta timu itakayompa maslahi bora zaidi, uamuzi huo unaonekana kuwachukiza viongozi wa Yanga, wanachama na mashabiki wao.

Jambo moja ambalo Yanga wanasahau ni kuwa: ” Sitaki mwenziwe basi”.  Feisal amesema sitaki tena Yanga hivyo ilikuwa ni busara ya kawaida kwa Yanga kukubali hali iliyotokea.

Pengine niwakumbushe wasomaji wa makala haya kuwa  klabu ya Simba iliwahi kumpoteza mchezaji kipenzi, Zamoyoni Mogella aliyekuwa kipenzi cha timu yao akajiunga Yanga mwaka 1992.

Kiwango cha uchezaji wake Zamoyoni Mogella kilikuwa kikubwa kiasi cha kupachikwa jina la “Golden Boy” siku hizo akitamba katika ulimwengu wa soka.

Simba ijapokuwa walinuna, lakini hawakufanya tafrani wala  hawakutishia kususia bidhaa za Abbas Gulamali.

Katika ulimwengu huu suala la mtu kutafuta maslahi yake binafsi si jambo la ajabu. Ni kawaida hata kwa wafanyakazi katika sekta mbalimbali wanatafuta maslahi bora zaidi kwa mustakabali wao.

Iweje leo iwe kiroja kwa mchezaji Feisal Salum kutafuta ahueni katika timu nyengine yazuke maneno, huku akitupiwa vijembe mtawalia na mashabiki wa Yanga tena wengine ni watu wazima wanaoweza kumjukuu?

Feisal hakuumbwa kucheza Yanga maisha, kila mmoja anahemea kwa upande wake kukitafutia hali iliyototonoka.

Ikumbukwe kuwa maisha ya wachezaji wengi baada ya kuacha soka yanakuwa magumu sana, sipendi kutaja majina, lakini jamii ya wanamichezo ni mashuhuda wa haya ninayoyasema.

Feisal Salum hataki kufanya pengine makosa ya watangulizi wake ya ” Wema wa Mshumaa” unafurahisha umati huku unateketea.

Feisal Salum hataki tena kugeuka mshumaa, kufurahisha umati huku akiteketea, anataka maisha bora zaidi na yenye kumuhakikishia kesho yake na baada ya kustaafu soka asigeuke kituko na kuwa mzigo katika jamii.

Hivyo basi, iwe itakavyokuwa iwe kuna mkataba au hakuna mkataba, suala la Feisal Salum  kuamua kwenda anakotaka kutafuta  ” mpunga zaidi ” ni jambo ambalo tungetarajia  watu wangechukulia ni suala la kawaida katika mambo ya soka.

Tunajiuliza nongwa hii kwa Feisal Salum inatoka wapi? Nini chimbuko lake?  Yanga ni timu kubwa na yenye mizizi na chimbuko na kamwe haiwezi kuyumba kwa sababu ya kuondoka Feisal.

 Washaondoka wengi na Yanga bado ipo sasa nongwa inakujaje?

Mimi nadhani kuna kila sababu ya uongozi wa Yanga kutumia busara zaidi kumuachia mchezaji huyo kutafuta maslahi yake.

Kumekuwa na kilio kwa wachezaji wazalendo kulipwa maslahi duni na timu zao za soka za hapa nchini, huku wachezaji wa kigeni wakilipwa fedha nyingi.

Viwango wanavyocheza wachezaji hao kutoka nga’mbo havitofautiani na kiwango anachocheza Feisal na pengine kwangu mimi Feisal Salum ni bora zaidi kuliko hao wanaoitwa wachezaji kutoka nje.

Wakati mashabiki wa Yanga wakimnanga Feisal ni muhimu wakumbuke mchango aliotoa ndani ya timu wakati wengi wa wanaopiga makelele hawana mchango wowote zaidi ya domo mtindi maziwa kwa mwenye ng’ombe.

Kimsingi Feisal Salum amefanya uamuzi wa busara kujitafutia maisha bora zaidi na kuachana na mambo ya ” Tumpambe kwa Maua:”  Huku yeye akiumia kwa jambo ambalo hakupaswa kuwa hivyo.

Mimi si mwanasheria, lakini mkataba wowote ule uweze kudumu ni lazima pande mbili au zaidi zilizotiliana saini mkataba huo kuendelea kubaki katika makubaliano hayo, ikitokea upande mmoja hautaki basi ndio mwisho wa mkataba huo.

Haiyumkiniki upande mmoja wa mkataba kulazimisha kutokuvunjwa mkataba kwa visingizio hivi na vile, Feisal Salum  keshasema ” Babajeni….

Yanga mwacheni Feisal Salum akacheze katika timu anayotaka kama ni chaguo lake, akiamini kuwa mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe.

Feisal yupo Unguja, amepoa hana makeke, akiamini kuwa kama sio uwezo wake Yanga wasingemshurutisha kubakia timu yao.

Msumari unapochoma ndipo unapotokea, Yanga walimchukua Feisal Salum kupitia mgongo wa Singida.

Feisal Salum alichukuliwa kwa njia ya hadaa kwenda Singida kwa nguvu za viongozi fulani serikalini ambako alikwenda kupinda na baadae kusajiliwa timu ya  Yanga.

Hivyo basi, kwa wazazi na walezi hatuna sababu ya kufanya nongwa, kununa, tumuache  Feisal Salum akacheze katika timu ya ndoto yake.

Marijan Rajab aliwahi kuimba ” Pesa Sabuni ya Roho” mwenye pesa akipita kila mtu anasimama, analosema ndilo linalopewa uzito hata kama la ovyo.

Nimalize kwa leo kwa kusema ” SITAKI MWENZIWE BASI “.

 

*Mwandishi ni Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar.

Habari Zifananazo

Back to top button